Rasilimali zote muhimu huwa zina uhaba au ukomo, hivyo zinapotumika eneo moja, haziwezi kutumika tena eneo jingine.
Rasilimali hizo zinaweza kuonekana kufanya vizuri kwa matumizi fulani, lakini zingetumiwa kwa namna nyingine zingefanya kilicho bora zaidi.
Unapoona kizuri na kukifurahia, unakuwa hujaona kilicho bora zaidi na hivyo hukipi uzito.
Chukua mfano wa rasilimali ya muda, muda wako una ukomo, lakini mambo ya kufanya ni mengi. Ni lazima uwe na vipaumbele, uchague kufanya mambo fulani na mengine uachane nayo.
Kwa wengi, huchagua ambayo ni mazuri, lakini wanaacha yale ambayo ni bora. Mfano kufuatilia habari mbalimbali, unaweza kufurahia kwa sababu unajua kila kinachoendelea. Lakini kuna vitu umeshindwa kufanya kwa sababu muda wako umeupelekea kwenye kufuatilia mambo.
Huenda ni kitabu umekuwa unapanga kuandika lakini hupati muda, huenda ni biashara umekuwa unataka kuanzisha au hata kitu fulani unataka kujifunza.
Unafurahia kujua kila kinachoendelea, lakini ambacho huoni ni kitabu ulichoshindwa kuandika, biashara ambayo hujaanzisha na maarifa ambayo hujajifunza.
Vyote hivyo ambavyo ni bora havionekani na hivyo huvipi uzito wa kutosha, lakini unafurahia kile ambacho umefanya na muda wako, ambacho hakina manufaa makubwa kwako.
Kila siku jifanyie tathmini ya kutambua ni yapi muhimu ambayo huyaangalii na hivyo kuwa kikwazo kwako. Kila siku pitia matumizi ya muda wako na ona wapi unaweza kuondoa muda wako sasa na kuweka kwenye yale ambayo ni muhimu zaidi.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye fedha, unaweza kutumia fedha zako kwa mambo yanayoonekana mazuri, lakini kuna ambayo ni bora zaidi yasiyoonekana ambayo ungeweka fedha zako huko ungenufaika zaidi. Na hapa kikubwa ni matumizi na uwekezaji, unaweza kununua vitu unavyotaka na utaviona, lakini hilo litakuzuia kuwekeza na kupata faida kubwa baadaye.
Kwa kila rasilimali uliyonayo, jua unaweza kuitumia vizuri au kuitumia kwa ubora. Matumizi mazuri yanaonekana haraka, lakini yaliyo bora huwa yamejificha. Lazima ujitathmini kwa kina ili upeleke rasilimali zako kwenye yale ambayo ni bora.
Ona yasiyoonekana lakini ni muhimu, ili uyape uzito wa kutosha.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Nitajizuia kutumia fedha zangu kwa mambo mazuri yanayoonekana kirahisi ili nizitumie kwenye mambo bora yasiyoonekana.
Shukrani sana Kocha.
LikeLike
Vizuri Datius kwa maamuzi haya muhimu.
LikeLike