Kwa kila aliyefanikiwa, huwa kuna mengi yanasemwa kuhusu wao.

Kuna hadithi nyingi watu watakuambia kuhusu waliofanikiwa.

Lakini nyingi ni za yale mambo yanayoonekana, ambayo siyo ukweli kamili kuhusu watu hao.

Iwe yanayosemwa ni mazuri au mabaya, siyo ukweli kamili.

Kuna mengi ambayo waliofanikiwa wanakuwa wamepitia ambayo hakuna anayeweza kuyaona na kuyaelezea.

Wakati mwingine hata wao wenyewe hawakumbuki mengi waliyowahi kupitia, maamuzi mbalimbali ambayo wamewahi kufanya na yakawa na mchango mkubwa kwenye mafanikio yao.

Kila aliyefanikiwa kuna vitu alichagua kupoteza na kipindi anafanya hivyo watu walimbeza na kumcheka, kuona hajui anachofanya. Hakutetereka wakati huo kwa sababu alijua nini anataka, akaendelea na hilo likapelekea kupata mafanikio makubwa.

Kila aliyefanikiwa aliweka kipaumbele kikubwa kwenye kazi kuliko mambo mengine. Wengine waliwasema vibaya kwenye hilo, wakiwaona hawana maisha mengine bali kazi au biashara zao na kwamba wamekosa kujali mambo mengine kama familia na mahusiano, lakini wao walijua kuna kipindi kazi na biashara zao zinawahitaji zaidi na kuwa tayari kujitoa katika vipindi hivyo.

Kila aliyefanikiwa aliweka kipaumbele kwenye kuweka akiba na kuwekeza badala ya kufanya matumizi ya kujionesha. Walipewa majina mengi, bahili, wagumu na kadhalika, lakini mwisho wa siku wamefanikiwa.

Kuna mengi mno ambayo huwezi kuyaona kirahisi kwa waliofanikiwa, lakini yamechangia mno wao kufika walipofika. Hivyo unapaswa kuwa imara sana kwenye safari yako ya mafanikio, uchague kuwapuuza wengine na yale wanayosema ili uweze kusimama kwenye kilicho sahihi kwako.

Kitu kimoja unachopaswa kujua ni kwamba kama utasikiliza na kufuata ushauri wa kila mtu, hutaweza kufanya jambo lolote kubwa kwenye maisha yako. Kwa sababu wengi walio tayari kukushauri kabla hata hujawaomba ushauri ni wale ambao hawajafanikiwa, na watakachokushauri ni kile ambacho wamesikia kutoka kwa wengine.

Hivyo jua kwa hakika kile unachotaka, jua gharama unayopaswa kulipa kukipata, tengenea mchakato wa kukifikia na weka mkazo kwenye mchakato wako huku ukiwapuuza wengi kwenye yale wanayosema.

Endelea kujifunza kila wakati na kuwa bora zaidi, endelea kujifanyia tathmini kila wakati na kuboresha mikakati yako kadiri unavyokwenda. Kama unataka kujifunza kwa wengine, jifunze kwa waliofanikiwa kwenye yale wanayofanya au waliyofanya na kwa ambao hawajafanikia kuepuka yale ambayo wamekuwa wanafanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha