Wakati taifa la Marekani linapeleka mtu kwa mara ya kwanza mwezini, hawakuwa na kompyuta yenye uwezo kama simu unayotumia sasa.
Vitabu bora kabisa tunavyosoma mpaka leo, viliandikwa zaidi ya miaka elfu mbili iliyopita, wakati bado watu wanaandika kwenye mawe na magome ya miti.
Viongozi bora kabisa walioendesha mataifa na taasisi zao vizuri, waliweza kufanya hivyo bila ujio wa kusambaa kwa habari haraka.
Sasa hivi tuna rasilimali nyingi, lakini tunashindwa kufanya hata kwa kiwango walichoweza kufanya wale waliokuwa na rasilimali chache kuliko sisi.
Hapo ulipo sasa, tayari una rasilimali za kutosha kufanya chochote unachotaka kufanya, lakini unachoangalia ni rasilimali ulizokosa.
Kweli kuna rasilimali muhimu unaweza kuwa huna, lakini kuna ambao waliweza kufanya wakiwa hawana hata rasilimali ulizonazo wewe sasa.
Hivyo acha kuwa mtu wa kutoa sababu na visingizio, kama kuna kitu unataka kufanya, kifanye sasa kwa rasilimali ulizonazo. Na kama unaona rasilimali hizo hazitoshi, basi achana nacho na fanya vingine unavyotaka, lakini usijidanganye wala kudanganya wengine kwamba kinachokukwamisha ni rasilimali.
Sayansi na teknolojia imekua sana, imechukua nguvu kutoka kwa wachache na kuipeleka kwa wengi, lakini wengi hao hawawezi kuitumia.
Mfano simu janja uliyonayo, ni kifaa chenye nguvu kubwa mno, unaweza kukitumia kujifunza chochote unachotaka na unaweza kukitumia kuandika au kurekodi sauti na hata video ya chochote unachotaka kufundisha.
Lakini hebu jiulize umekuwa unatumia kifaa hicho kufanya nini? Kwa sehemu kubwa ni kupoteza muda kwa mambo yasiyo muhimu na manufaa yoyote kwako. Unahangaika kutafuta muda na vitu vya kufanya, wakati muda ulionao tayari unautawanya hovyo.
Kwa kila unachotaka kufanya, anza kujikagua mwenyewe ni rasilimali zipi ulizonazo unazoweza kuzitumia kukamilisha hilo. Zipo nyingi, wewe mwenyewe utashangaa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,