Mazoea ni tabia, pale unaporudia rudia kufanya kitu, akili inakariri na hivyo unajikuta unaweza kukifanya bila hata ya kufikiri.

Kuna mambo mazoea ni mazuri kwa sababu inapunguza mzigo kwa akili kufikiri kila jambo. Mfano shughuli ndogo ndogo na za kawaida unazofanya kila siku.

Lakini kuna mambo ambayo ukiweka mazoea tu unakuwa umepoteza.

Chochote kile ambacho unataka kufikia mafanikio makubwa, unapoweka mazoea ndiyo unakuwa umechagua kutokufanikiwa.

Kwa sababu unapofanya kwa mazoea maana yake hujifunzi tena, unafanya kile ambacho ulifanya jana ambacho pia ndiyo ulifanya juzi na juzi nyingine tena.

Eneo unalotaka kufanikiwa unapaswa kuwa unakua kadiri siku zinavyokwenda.

Na ili ukue lazima ujifunze vitu vipya na kuchukua hatua za tofauti, ujaribu vitu vipya.

Angalia ni mazoea gani ambayo umeshajijengea kwenye maeneo muhimu kwako, iwe ni kwenye kazi au biashara, kisha weka mkakati wa kuvunja mazoea hayo.

Jisukume kujifunza vitu vipya na kila kipya unachojifunza kiweke kwenye matendo. Siyo yote unayojaribu yatafanikiwa, lakini machache yatakayofanikiwa yataleta matokeo makubwa na ya tofauti.

Jikamate kila unapojiambia umeshazoea na utafute ukuaji zaidi kwenye kila eneo la maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha