Huwa tunahangaika na kujisumbua na mambo ambayo bado hayajatokea, kwa kutabiri namna ambavyo mambo yatatokea.
Lakini mara zote dunia hutushangaza, kwani kinachokuja kutokea ni tofauti kabisa na tulivyokuwa tunategemea na hivyo kuhofia.
Mifano ni mingi uliyonayo kwenye maisha yako, ya mambo ambayo ulihofia sana, lakini yakaja kutokea tofauti na ulivyotegemea. Na hata yalipotokea kama ulivyotegemea, madhara hayawi kama ulivyotegemea.
Hivyo njia bora ya kuwa na maisha tulivu na bora ni kujua huna uhakika wa chochote unachohofia na dunia ina mengi mazuri kwa ajili yako ambayo bado hujayaona.
Kila unapokuwa na hofu na yajayo, jua fika kwamba hofu hiyo umejitengenezea mwenyewe na siyo uhalisia ulivyo, kwa sababu hujui hata kitakachokuja kutokea ni nini.
Mara zote tegemea mazuri kutokea na hata kama yatakayotokea siyo mazuri, jua kuna namna nzuri ya kuyatumia kwa manufaa yako.
Usipoteze nguvu zako kuhofia mambo ambayo huna uhakika nayo, jua yatakayokuja kutokea ni tofauti kabisa na unavyotegemea.
Hakuna awezaye kutabiri chochote ambacho hakijatokea kwa uhakika wa asilimia 100. Hata wale waliosomea na kubobea kwenye eneo husika, bado utabiri wao hauwi bora. Hiyo inatuonesha ni jinsi gani dunia ina mengi tusiyojua, tukichagua kuwa wanyenyekevu na kupokea kama yanavyokuja, maisha yetu yatakuwa bora sana.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,