Asili ina kanuni zake nyingi, huwezi kupanda mbegu na kuivuna hapo hapo ukaila. Lazima uwe na subira, lazima uipe mbegu hiyo muda, ikue, izae mbegu nyingi zaidi ndipo uvune na kuweza kula.

Sasa pata picha umekuwa unaona shamba liko mahali, lina rutuba nzuri na hakuna anayelilima. Unaona unaweza kutumia shamba hilo, unalima na kupanda mbegu. Unapalilia na kuweka mbolea, mazao yametoka vizuri na una matumaini mavuno yatakuwa mazuri.

Siku ya kuvuna inafika, unakwenda kuvuna ukiwa umejiandaa kubeba mazao mengi, unafika shambani na kukuta shamba limewekewa ulinzi. Unauliza na kuambiwa huruhusiwi kuingia kwenye shamba hilo, mwenyewe amekataza yeyote yule asiingie.

Unaeleza kwamba wewe ndiye uliyelima shamba, umepanda mbegu, umepalilia na kuweka mbolea, una haki ya kuvuna mazao yako hata kama shamba siyo lako. Unaulizwa je una hati ya shamba? Je kuna makubaliano uliingia na mwenye shamba kwamba utalitumia kulima?

Unabaki huna majibu, kazi yako yote uliyoiweka, subira kubwa uliyokuwa nayo imepotea bure, hupati chochote.

Unaweza kuona mfano huu ni kitu ambacho hakiwezi kutokea, lakini nikuambie jambo moja, ni kitu kinachotokea kila siku. Watu wengi sana wanalima kwenye mashamba ambayo hawana umiliki nayo. Na mfano mzuri ni mitandao ya kijamii.

Kama unatumia mitandao ya kijamii unajua ni jinsi gani unaweka juhudi kubwa kwenye kuweka maudhui mbalimbali, iwe ni maandishi, picha, sauti au video. Unapambana kweli kupata wafuasi wengi kwenye mitandao hiyo. Unaweka muda na juhudi, unakuza mtandao wako kweli halafu siku moja unaambiwa akaunti yako kwenye mtandao huo imefungwa au kuzuiliwa.

Juhudi zote ulizoweka zinayeyuka, huna pa kwenda kushitaki, maana huna umiliki wowote kwenye mitandao hiyo.

Ndiyo maana nimekuwa nawasihi sana wale wote wanaotoa huduma za mafunzo mbalimbali, kutokutegemea mitandao ya kijamii pekee. Unapaswa kuwa na shamba unalolimiliki mtandaoni na sehemu ya uhakika ni kuwa na blog yako ambayo unailipia kuhifadhi maudhui yako yote.

Kwa njia hiyo hata kama wale wanaokuhifadhia maudhi yako watataka kukunyima huduma hiyo, unapakua maudhui yako yote na kuyahamishia sehemu nyingine. Hapo unakuwa kama umekodi shamba na kulima, mwenye shamba akikuambia hataki kukukodishia tena, hawezi kuchukua mazao yako.

Kwa kila juhudi unayoweka, hakikisha unalinda mavuno yake ya baadaye. Kuna wengi wanakutega uweke juhudi sasa, halafu mavuno yanapofikia wanakugeuka na hupati chochote.

Hata kwenye kazi na biashara unazoshirikiana na wengine, mwanzo mnaweza kuanza na nia njema, ukijua kila mmoja atajali maslahi ya mwenzake, unaweka juhudi kubwa, mafanikio yanaonekana lakini hufaidi matunda ya mafanikio yako.

Usiishie tu kuweka juhudi, bali linda kila juhudi unayoweka ili uweze kufurahia matunda yake baadaye.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha