Chetan Bhagat ni mwandishi toka nchini India akiwa mbobezi wa uaandaji wa vitabu na mtunzi wa vitabu vya riwaya vipatavyo 5 hii ilikuwa mwaka 2012. Moja ya kazi zake za riwaya zimetumika katika bodi kubwa za uaandaji wa filamu nchini India ya “Bollywood”. Hapa kuna jambo kubwa la kujifunza kwa nchi yetu ( Tanzania ) kuwa pawe na mfumo wa waandishi wa kazi za riwaya zikawaleta wasanii na waigizaji pamoja kama ilivyo kwa mwandishi Chetan Bhagat na ‘Bollywood’. Mbali na uandishi ambao ulikuja kasi baada ya kuacha kazi yake katika masuala ya kibenki pia alijikuta anakuwa mhasamasishaji na mzungumzaji kisha kupewa fursa ya kuandika katika magazeti na gazeti kubwa huko nchini India ili kazi zake zienee kwa watu wengi ambao wamekuwa wakimfuatilia hasa vijana. 

Anaandikwa na kampuni ya Fast Company iliyopo nchini Marekani kama moja ya watu 100 wabunifu wakubwa duniani na jarida la TIME lilimwandika kama moja ya watu 100 wenye ushawishi mkubwa Duniani. Aina ya uandishi wake ni uandishi wa hisia na wenye kukufanya ufikiri ulipo, uangalie hali ilivyo na pia kuona picha ya mbele ya vizazi vingine vitakavyokuja siku zijazo. Mwisho kabisa wa kitabu anashirikisha hadithi fupi 2 za mafunzo na nitakushirikisha hadithi moja ambayo nimeisoma mara mbili mbili ni juu ya BATA na MAMBA baada ya kumaliza kujifunza mambo 20 ambayo nimejifunza ili usome nawe na kuona namna ya kuyatumia.  

Ndani ya kitabu hiki kimegawanyika katika sehemu 5; Sehemu ya kwanza ni ya kuelezea historia ya maisha ya mwandishi namna alipotokea huko Delhi nchini India, maisha yake jinsi ambavyo yalikuwa duni na umaskini ilikuwa ni wimbo ambao ulikuwa maarufu katika familia yao. Historia inagusa maisha ya shule, kupata kazi na hadi kuacha kazi na kujiwekeza katika uandishi, uhamasishaji na uandishi wa makala gazetini na mwisho uandishi wa kitabu hiki cha picha ya namna mabadiliko ya nchi yanahitaji kumtazama kijana kwa mapana kama mihimili ya taifa lolote Duniani. 

Ya pili ni juu ya jamii namna maisha yalivyo na kijana anataka nini na kupaswa kufanya nini. Eneo la 3 ni juu ya masuala ya siasa na nne ni juu ya KIJANA na mwisho eneo la 5 ni hadithi fupi 2 za kujifunza na ndoto ya India anayotamani kuja kuiona. 

Karibu nikushirikishe mambo 20 ambayo nimejifunza juu ya kitabu hiki na kama kijana basi umakini uwe mkubwa na kama u mzazi basi weka akiba kwa kijana wako. 

  1. Mashuleni tumefunzwa juu ya historia za watu mashujaa ambao kwa namna moja wamesaidia jamii zetu kufika hapa tulipofika. Lakini je tumewahi jiuliza pia ni kwa namna gani baadhi ya maamuzi yao ya nyuma yametugharimu sisi kufika hapa?

2. Kwanini Taifa ni maskini ?. Hili swali mwandishi alikuwa akijiuliza kwa upande wa nchi yake India. Lakini kabla ya kuuliza kwanini nchi ni maskini sharti uanze na mduara wa kwanza kwako kwa nini wewe sio tajiri au huna utajiri?

3. Rushwa ni adui wa maendeleo Duniani kote si pekee India. Rushwa ni moja ya mambo ambayo yanakwamisha kuendelea kwa mataifa mengi Duniani.

4. Ukisimamia ukweli na wengine hawako hivyo unayo hatari lakini usiogope maana mabadiliko ya jamii yanaanzia msingi wa kujulikana kweli ya mambo. 

5. Wanasiasa ni zao la jamii na walivyo ni picha ya jamii yao ilivyo pia. Kabla ya wanasiasa kulaumiwa swali lianze ngazi ya jamii ya hao wanasiasa ikoje ?

6. Mifumo inayoongoza jamii kama ni mibovu itaendelea kuitesa jamii mpaka mifumo hiyo ibadilishwe ndipo njia ya kutoka itapatikana 

SOMO la KUIGA; Mwandishi anatumia mfano wa nchi ya Marekani ambayo imeshajitengenezea mfumo wa watu wake kuwa Utajiri ni zao la JUHUDI, UGUNDUZI, VIPAJI na BIASHARA. Hivyo watoto wanazaliwa na hata shule zao zinahimiza watu kuweka Juhudi, kuwa wabunifu na wagunduzi na kunoa vipaji vyao. Nje na hapo unayo hatari ukifanya mambo kwa njia za udanganyifu. Huu mfumo mzuri unaopaswa kujengwa maeneo mengi Duniani kuwa njia ya Utajiri sio bahati nasibu ni KAZI, tena KAZI NZITO. 

7. Unaweza kupata fedha kwa njia zisizo kihalali lakini maisha ya namna hii mwisho wake ni aibu na fedheha. 

8. Maradhi ya mtizamo (Attitude Sickness) ndio yanayomaliza maisha ya ndoto za vijana zisiweze kufanikiwa. Ukijawa na mtizamo hasi mafanikio yatakaa kando nawe. 

9. Siasa haifai kugawa watu bali iuanganishe watu kwa maslahi ya taifa. 

10. Vijana wadogo wafundishwe mambo ya nchi zao na kutayarishwa kushika nchi siku zijazo 

11. Ukimya wa wanasiasa pahali pa kuongea si ujasiri ni kunyima haki ya wale ambao wamewapa nafasi za muda kwao kuwa viongozi

12. Watu wanaochaguliwa kwenda katika vyombo vya kufanya au kutoa maamuzi (Bunge) je wanastahili kuwa pale kwa niaba ya jamii walizotoka ?

13. Fedha zitakazo tumika kununua silaha hazitarejeza fedha bali fedha ambazo zinaenda kutumika kuboresha miundo mbinu zitaongeza ubora wa maisha ya watu. 

14. Jamii ina nafasi ya kuwakumbusha viongozi wao kuwa wako katika nafasi za uongozi pana kazi nyingi za kufanya na wawe tayari kufanya na si kujitazama kimaslahi yao binafsi. 

15. Jamii haiendelei kwa kuendelea kulaumu historia ya nyuma ya maamuzi mabovu ya watangulizi bali ni ile yenye kuandaa leo kwa kutengeneza kesho nzuri ya vizazi vingine. 

16. Kipaji ni hazina kubwa ya taifa lolote Duniani. Wale wenye vipaji wakipewa ulezi mzuri ni hazina ya taifa na utambulisho wa taifa lolote lile Duniani. Watu kama hawa Mbwana Samatta kwa kipaji chake cha mpira kabeba utambulisho mkubwa wa taifa la Tanzania. 

17. Vijana ili wawe na nguvu moja sharti washikane mikono na kuwa tayari kujenga taifa kwa kuanza kujijenga wenyewe kimtazamo, kifikra na kiuchumi. 

18. Kwa njia ya kujifunza na pia walojifunza wakafunza wengine ndivyo taifa bora huzaliwa na lenye maendeleo makubwa ndani ya muda fulani kupita.

19. Jamii inayopuuza kutoa elimu bora kwa vijana wake inajipuuza yenyewe na kukaribisha jamii ya watu wajinga na katika ujinga umaskini haukosekani.  

20. Amani ya jamii au taifa ni kichocheo kikubwa cha watu kuwa na nafasi ya kufanya kazi na kufanya shughuli za maendeleo. 

Hadithi niliyokuahidi kukusimulia; 

Katika kijiji kimoja kilichokuwa juu ya kilima. Kijiji hiki kilikuwa na kila kitu isipokuwa jambo moja ambalo lilikuwa ni ukosefu wa maji. Upatikanaji wao wa maji ulitegemea zaidi makusanyo ya maji ya mvua ambapo mvua za msimu zilipopata kunyesha. Juu ya kilima katika kijiji kilicho kuwa katika kilima palikuwa na bwawa dogo ambalo ndilo wao walikuwa wakitegemea kujipatia maji. Kila mvua iliponyesha ilibidi wakusanye maji katika ndoo zao na kujaza katika bwawa hili dogo. Katika siku kupita bwawa hili likapata ugeni wa bata na hata kuwa eneo la kupumzika kwa wanakijiji hata watoto. Bata hawa walikuwa ni bata dhahabu ambao uwepo wao ulifanya bwawa livutie sana hasa kwa watoto hata kiasi bata kuwavuta watoto wapende kuogelea humo. Siku nyingi hazikupita bata walipata ugeni wa bata mwenye hekima aliye pata naye kuwa katika familia hiyo ya bata wa dhahabu. 

Baada ya muda pakatokea kutoweka kwa watoto watatu katika mazingira ambayo yalileta mashaka kwa wanakijiji hata wasiwaone hao watoto. Na ndani ya wiki nyingine zilizofuata idadi ya watoto ikaongezeka na kutia hofu zaidi. Kupatikana kwa mifupa ya watoto kando ya bwawa kulitia shaka kubwa zaidi kuwa huenda ndani ya bwawa pana mamba. Lakini walipohoji kwa bata mwenye hekima akasema huenda watu toka nje ya kijiji ndio wanaofanya hivyo. Hivyo wakayaamini maneno ya bata mwenye hekima. Lakini kupotea kwa watoto kulizidi idadi kila mchana ulipokuwa ukiisha ndipo kijiji kikakubaliana kuweka uangalizi mkubwa wa eneo la bwawa na katika usiku mmoja wakiwa katika nyumba zao wakasikia kelele toka bwawani na kukimbia kwenda kuona wakaona ni mamba ambao walikuwa wakicheza, na hata kutaga mayai ndani ya bwawa huku kando bata wa dhahabu walikuwa kando ya bwawa kuna pango ambalo walikuwa wakiishi. 

Kijiji kikaamua kuanza kuchimba eneo lingine kuandaa maeneo ambayo wataweza kuandaa maeneo ya maji na makachimba mabwawa na huku kule katika bwawa la zamani wakapitisha njia ya kutoa maji ya bwawa na walichokiona ni wingi wa mamba na chini ya miguu ya bata mwenye hekima. Kwa kuwa maji ni uhai basi viumbe wote wa bwawa hili la zamani wakafia wote humo. Habari ya bwawa jipya walojenga likawekewa wigo na likawa salama kwa kijiji na hata watoto kwenda. 

Funzo la hadithi ni umuhimu wa kujifunza kudadisi, kuhoji na kujua ukweli kama namna ya kuikomboa jamii. Mafunzo ya kitabu hiki ambacho mwandishi aliandika kwa vijana wa India ila kina mafunzo yanayoakisi pia maisha ya nchi za Kiafrika ya vijana, jamii na tawala zake.

Mchambuzi wa Kitabu

Dkt. Raymond N Mgeni

+255 676 559 211

raymondpoet@yahoo.com