Uliwahi kufanyika utafiti kwa wale wanaofanya utapeli. Utafiti huo ulitaka kujua iwapo watu wanaofanya hivyo hawasutwi nafsi zao kwa kuwaibia na kuwatapeli wengine.
Mmoja wa watu waliohojiwa kwenye utafiti huo alitoa jibu ambalo liliwafanya watafiti wapate mtazamo ambao hawakuwa nao awali. Mtu huyo aliwaambia ni kweli tabia ya utapeli inamuumiza yeye mwenyewe, lakini njaa inaumiza zaidi.
Uhitaji wa fedha umekuwa unatumika kama sababu ya kuhalalisha mambo ya hovyo ambayo watu wanafanya. Mtu anaona ni sahihi kuiba kwa sababu ana njaa na hajui atapata wapi chakula. Mwingine anaona ni sahihi kuchukua rushwa kwenye kazi yake kwa sababu kipato ni kidogo na hakitoshelezi.
Ni rahisi kuona hayo ni sahihi, hasa unapokuwa unaangalia muda mfupi. Lakini unapoangalia kwa muda mrefu, unaona mambo hayo yana madhara makubwa ya baadaye kuliko manufaa ya muda mfupi yanayopatikana.
Chukua mfano wa wezi, matapeli na wachukua rushwa, baadaye hiyo huwa ndiyo tabia yao. Wanajikuta hata wafanye nini hawaridhiki, wanazidi kufanya mambo hayo zaidi.
Mahitaji yako ni muhimu, lakini usikubali njaa ya siku moja ikufanye ubaki kuwa duni maisha yako yote. Zipo njia nyingi sahihi za kutoka popote ulipokwama, ila njia hizo zinahitaji sana uvumilivu na kujipa muda. Utapitia mateso makubwa kwa kipindi kifupi, lakini baadaye utakuwa umejenga msingi utakaokuondoa kabisa kwenye hali hiyo.
Lakini kufikiria kwa muda mfupi, kumewafanya wengi kuchukua hatua ambazo zina madhara kwao, usikubali hili litokee kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante Sana kocha.
LikeLike