Kila mtu huwa ana madhaifu yake, ni wale wanaoyatambua na kuhakikisha hayawi kikwazo kwao ndiyo hufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yao.
Wale wanaoyakataa madhaifu yao huwa ni kiburi tu walichonacho au ujinga wa kutokujitambua, lakini huwa hawafanikiwi. Kwa sababu hata wapate fursa nzuri kiasi gani, madhaifu yao huwa kikwazo.
Kila mmoja wetu anawajua watu kwenye maisha ambao wana bahati ya kupata fursa nzuri, iwe ni kazi inayolipa vizuri au mtaji wa kuanza biashara kubwa, lakini watu hao wanazichezea fursa hizi na kuzipoteza. Hata baada ya kupoteza fursa nzuri, bado wanapata nyingine nzuri zaidi, nazo pia wanazipoteza.
Wengi wa watu hao wanakuwa na madhaifu ambayo huwa yanakuwa kikwazo kwao, kwa kutokuyatambua au kuyapuuza yanakuwa yanaingilia kila fursa nzuri wanayoipata.
Huenda na wewe unayewaangalia watu hao na kusema ungepata fursa kama zao ungefanya makubwa, una madhaifu yako ambayo hujayajua au unayapuuza na hivyo ukipata fursa hizo utazipotea. Au pia kuna fursa ulishazipata na kuzipoteza, kuna wengine wanatamani wangepata fursa kama zako.
Kwa upande mwingine, tunapaswa kuyatambua madhaifu ya wale tunaoshirikiana nao na kuona namna bora ya kuyazuia yasiwe kikwazo kwenye ushirikiano tunaotaka kuwa nao. Hili linaanzia kwenye mahusiano ya karibu kama ya ndoa, mwenza wako ana madhaifu yake, unapoyajua inasaidia kuishi naye vizuri.
Kadhalika kwenye kazi na biashara, kila unayejihusisha naye, iwe ni mwajiri wako, bosi, mfanyakazi wako au mshirika wako wa kibiashara, kuna madhaifu wanayo. Ni wajibu wako kuyajua na kuona njia bora ya kushirikiana nao ili madhaifu yao yasiwe kikwazo.
Kuyaendesha maisha yako ukitegemea kukutana na aliyekamilika ni kujizuia kufanikiwa, kwa sababu mtu wa aina hiyo hayupo, anaweza kuingiza utakavyo kwa siku chache, ila baadaye hataweza kuendelea na maigizo hayo, hivyo utauona uhalisia wake.
Kujitambua sisi wenyewe na kuwajua wale tunaoshirikiana nao ni hitaji muhimu sana kwenye mafanikio, lipe uzito wa kutosha.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante Sana kocha kwa makala nzuri, hakika kila mmoja anayo madhaifu yake,neno hilo au sentensi hiyo imezungumzwa vizuri ktk Kitabu cha Fungate ya milele,na mwalimu Hamisi kibwana Msumi,pia na wewe hapo juu umeigusia vizuri katika mahusiano, Ndoa,Wenza wanatakiwa kujua uimara na udhaifu wao.
LikeLike
Karibu Beatus.
LikeLike