Mwekezaji bilionea Warren Buffett amewahi kusema kinachopelekea maanguko ya uchumi ni tabia ya watu kufuata kundi.

Anasema watu wengi huwa hawawezi kutulia pale wanapoona kundi kubwa la watu likifanya kitu, huwa hawataki wapitwe, hivyo hukimbilia kufanya na kuishia kuanguka.

Ndiyo maana watu wengi hununua hisa wakati zinapanda bei na kuziuza wakati zinashuka bei. Wanapata hasara katika hilo lakini hawawezi kujizuia maana wanafuata kundi.

Hivyo ndivyo wengi wanavyoendesha maisha yao,

Waangalie wengi walio kwenye taaluma au kazi fulani, ni wachache mno waliochagua kwa sababu walitaka kweli, wengi walifuata kundi.

Angalia pia walio kwenye biashara, ni wachache mno wanaingia kwenye biashara wakijiambia wana thamani ya tofauti wanayoipeleka sokoni. Wengi mno wanaingia kwenye biashara kwa sababu wameona wengine wanafanya biashara hiyo na hivyo kuamini inalipa.

Wengi wametapiliwa na kuingia kwenye uwekezaji usio sahihi kwa sababu tu wameona wengine wananufaika na uwekezaji huo.

Ukishajikuta unafanya maamuzi kwa kutumia wengine, jua fika maamuzi hayo siyo sahihi kwako. Kama sababu ya kufanya kitu ni kwa sababu umeona wengine wanafanya, jua tayari umeshapoteza.

Hiyo ni kwa sababu hutakuwa na cha tofauti unachotoa, ni kama unasema na mimi pia nipo na hivyo kutegemea huruma ya wengine. Sasa inapokuwa kuna utitiri wa wengi wanaofanya kitu, huruma haitakusaidia.

Fanya maamuzi kwa kujitambua mwenyewe na kujua unachotaka, fanya maamuzi kwa sababu kuna cha tofauti unakwenda kufanya au kutoa, tofauti na hapo, maamuzi hayo hayatakuwa na manufaa kwako.

Ukiacha kuwatumia wengine kwenye maamuzi, utafanya maamuzi ambayo ni bora, kwa sababu utajisikiliza na kufanya maamuzi ya kweli.

Maamuzi ya kuangalia wengine yamejaa uongo mwingi, wengi watakuambia wananufaika na kitu wakati siyo kweli. Hakuna anayependa kukiri kwamba anachofanya hakimpi manufaa, hivyo wengi hudanganya, katika kudanganya kwao wanawaingiza wengi mno kwenye shimo.

Ni sawa na uingie kwenye fursa fulani ya biashara au uwekezaji baada ya kusikia mtu anahojiwa kwenye vyombo vya habari na kueleza manufaa yake kwenye eneo hilo. Jua kabisa katika hali hizo, kuna ukweli mwingi ambao watu hao hawatausema, hivyo unapofanya maamuzi kwa taarifa chache wanazokupa, yatakuumiza sana.

Na hata kama watu wananufaika kweli na kitu fulani wanachofanya, siyo tiketi ya uhakika kwamba na wewe ukifanya utanufaika kama wao. Lazima ujisikilize wewe mwenyewe, lazima kitu kitoke ndani yako kweli ndiyo kikunufaishe na siyo tu kuona wengine wanafanya na wewe utake kufanya halafu utegemee kufanikiwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha