Wanasheria huwa wana msemo kwamba kutokujua sheria siyo kinga ya kutokuhukumiwa na sheria hiyo.

Unaweza kuona hilo siyo sawa, lakini ndivyo asili inavyofanya kazi.

Maisha yetu yote, tumekuwa tunajifunza kwa kujaribu na kukosea, maana hiyo ndiyo njia pekee tunayoielewa.

Ulipokuwa mtoto uliimbiwa sana usichezee moto, lakini hukusikia, mpaka siku ulipokuunguza ndiyo ukashika adabu. Huenda ulikatazwa sana usichezee wembe au vingine vyenye makali, lakini hukuona uzito wa hilo, mpaka ulipojikata ndiyo ulielewa unaelezwa nini.

Hivyo ndivyo asili inavyoendesha mambo yake, asili ina sheria zake nyingi mno, ambazo haziko wazi ili mtu uweze kuzijua, ni mpaka utakapozivunja, upate maumivu ndiyo ujue kuna sheria kwenye jambo hilo.

Mfano unaona ndege wanaruka angali, unajiambia kwa nini na wewe usijaribu kuruka, unapanda kwenye mti mrefu na kujirusha, ukifika chini, maumivu utakayoyapata hutarudia tena.

Sasa unaweza kuona mfano huo wa kuruka kama ndege ni wa kijinga, kwa akili zako huwezi kufanya hivyo. Lakini kuna mengi umekuwa unafanya kwa namna hiyo kwenye maisha na asili imekuadhibu sawasawa.

Kwa kila tatizo, changamoto au kikwazo unachopitia kwenye maisha, jua kuna sheria ya asili umeivunja. Na asili inakuadhibu kwa changamoto na vikwazo mpaka uelewe na kufanya kilicho sahihi.

Kama umejikuta kwenye madeni, jua kabisa umevunja sheria ya asili. Sheria ya asili inasema upande kabla hujavuna, wewe unafikiri una akili sana kuliko asili, unaanza kuvuna kabla hujapanda na utatumikia adhabu ya madeni yenye riba mpaka akili ikukae sawa.

Changamoto za kazi, biashara, mahusiano, afya na kadhalika, huwa zinaanzia kwenye kuvunja sheria za asili, iwe kwa kujua au kwa kutokujua, iwe ni wewe mwenyewe au jamii nzima.

Asili inatufundisha kila siku, ila kwa adhabu na maumivu, kibaya ni kwamba tumekuwa hatulipati somo, tunapeleka hasira zetu kwenye maeneo yasiyo sahihi na asili inaendelea kutuadhibu bila huruma.

Tatizo la asili ni kwamba haitakuambua kuna sheria hii unavunja, yenyewe inashusha adhabu tu. Upo kwenye kazi ambayo huthaminiwi na wala hulipwi vizuri, unaweza kumlalamikia mwajiri wako utakavyo. Lakini rudi tu kwenye asili, dhahabu na chuma yote ni madini, lakini angalia bei ya kilo moja ya dhahabu na kilo moja ya chuma, ipi ghali? Asili inakupa somo la wazi hapo, chenye thamani zaidi kina gharama kubwa zaidi. Hivyo kama na wewe unataka ulipwe zaidi, kuwa wa thamani zaidi kwa kufanya vitu ambavyo wengine wanavihitaji zaidi.

Biashara yako inapata hasara kila wakati, unaweza kulalamikia hali ya uchumi, washindani, wasaidizi au chochote utakacho. Ila asili itaendelea kukuadhibu kwa kukupa hasara mpaka utakapojifunza sheria za asili na kuzifuata kwenye biashara. Sheria kwamba biashara lazima iwe na huduma au bidhaa ambayo watu wanaitaka na wako tayari kuilipia, iwe na wateja ambao ni waaminifu kwenye biashara hiyo na faida inayopatikana ni kubwa kuliko gharama zote zinazoingia kwenye biashara. Tofauti na hapo, utalalamika utakavyo, lakini mwisho wa siku utaambulia hasara.

Tukichagua tu kujifunza kutoka kwenye asili, tutapunguza vikwazo na changamoto nyingi mno kwenye maisha yetu.

Kwa kila unachokabiliana nacho kwenye maisha, kabla hujaendelea, hebu kwanza rudi kwenye asili, angalia asili inafanyaje kazi, utapata majibu ya sheria ipi unaivunja.

Nimalizie kwa kukupa mfano huu mzuri mno kutoka kwenye asili. Miti inayoona kwenye kivuli cha miti mingine mikubwa, huwa haipati jua la kutosha na hivyo haikui haraka. Inakua taratibu mno, lakini inakuwa imara. Na inapokuwa mikubwa hata nguzo au mbao zake huwa imara zaidi na thamani yake kuwa kubwa.

Miti inayoota eneo la wazi, huwa inapata jua la kutosha, inakua haraka sana lakini haiwi imara, hata inapokomaa, mbao zake huwa siyo imara, zinashambuliwa haraka na wadudu na haziwi na thamani kubwa.

Umeiona sheria ya asili hapo? Kama hujaiona ni hii, kinachokua taratibu kinakuwa imara na kudumu. Kinachokua haraka haraka kinakuwa dhaifu na hakidumu. Ukitaka kujipa mifano mingine, angalia mpapai na mbuyu.

Mifano ni mingi, sheria za asili ziko wazi, ila hakuna atakayekuambia hizo ni sheria unazopaswa kuzifuata bila kuvunja, ila utakapozivunja, adhabu utaipata kisawasawa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha