Kama kuna kauli yenye nguvu na maana kubwa kwenye maisha yetu ni kauli kwamba hakuna kipya chini ya jua.
Na ili kuwa sahihi zaidi, kauli hiyo inapaswa kuwa hakuna tatizo jipya chini ya jua, matatizo yamekuwa ni yale yale, ila yanakuja kwa njia tofauti na hatua tunazochukua kuyatatua ndiyo zinaweza kuwa tofauti.
Afya, chakula, mali, mahusiano, kazi/biashara, maana ya maisha na uongozi ni mambo ambayo yamekuwepo tangu enzi na enzi. Kila enzi zinakabiliana na mambo hayo kwa namna yake.
Kuna teknolojia mpya zinagunduliwa kila siku katika kukabiliana na matatizo haya ambayo tumekuwa nayo, lakini kitu kinachofanya kazi na kuleta matokeo ya uhakika ni njia ambazo ziligunduliwa tangu zamani, ambazo zimefanya kazi miaka na miaka.
Mfano kuna teknolojia nyingi mno za kutibu kila aina ya maradhi, lakini kitu chenye ufanisi mkubwa kabisa ni kujikinga usipate maradhi, ambazo njia za kufanya hivyo zimekuwepo tangu enzi na enzi.
Kuna mbinu mbalimbali za kuongeza kipato na aina nyingi za uwekezaji, lakini njia ya uhakika ni kutoa thamani na kuhakikisha matumizi hayazidi kipato huku ukiwekeza mahali panapozalisha.
Kuna mifumo mingi ya imani, dini na falsafa mbalimbali, lakini msingi mkuu kwenye kuwa na maisha tulivu ni kujitambua, kuwa na upendo na kuwa na shukrani, vitu ambavyo vimekuwa vinafundishwa miaka na miaka.
Hii ni mifano michache, lakini angalia tatizo au changamoto yoyote unayokabiliana nayo sasa, kisha rudi miaka 1000 mpaka 2000 nyuma na ona walikabilianaje nayo, utapata njia ya uhakika zaidi ya kukabiliana na tatizo au changamoto yako.
Matatizo ya wanadamu ni yale yale, yamekuwa yanajirudia kwa kila zama na kila kizazi, uzuri ni njia za kuyatatua zipo na zimekuwa zinafundishwa tangu enzi na enzi. Ni sisi kuzitafuta, kuzijua na kuzitumia kuweza kukabiliana na chochote tunachokutana nacho kwenye maisha.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,