Njia pekee ya kujenga uaminifu kwa wengine, kwenye jambo lolote lile ni kuwa mkweli, kusimama kwenye ukweli.

Mara nyingi watu hudanganya kwa nia njema, kwa kuona wakitoa ukweli mapema wanaweza kuwaumiza watu.

Lakini ukweli haujawahi kushindwa, ukweli hujitokeza hadharani tu, hivyo kuuficha sasa kwa sababu hutaki watu waumie, hujawazuia kuumia, wataumia ukweli utakapokuwa wazi, lakini pia wataacha kukuamini.

Hivyo chochote unachofanya kwenye maisha, kiwe kikubwa au kidogo, simamia kwenye ukweli. Siyo wote watakaopenda msimamo huo, lakini ndiyo msimamo pekee utakaokuletea watu sahihi.

Uzuri ni kwamba, ukweli tayari watu wanakuwa wanaujua, ila hakuna anayeusema, hivyo unaposimama kwenye ukweli, walio sahihi watakuamini kwa sababu umewapa sauti.

Ni pale ukweli unapokuwa mgumu ndiyo unahitajika zaidi kuusimamia, kwa sababu huo ndiyo wakati wengi wanaukimbia, hivyo unapousimamia unakuwa unatoa thamani ambayo watu hawaipati kwingine.

Kuficha ukweli kunaweza kukupa manufaa ya muda mfupi, lakini unapoteza kitu chenye thamani kuliko manufaa hayo uliyopata, ambacho ni uaminifu. Uaminifu unaweza kukufanya ukose fursa fulani, lakini utakuwezesha kupata fursa kubwa zaidi baadaye.

Uaminifu ndiyo sera iliyo bora kuliko zote, ni kauli iliyowahi kutolewa na Benjamin Franklin, kitu ambacho ni sahihi kabisa, msingi ambao unaweza kuyajenga maisha yako hapo na ukafanikiwa sana.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha