2277; Kuchaji Betri ya gari…

Kama una uelewa kidogo kuhusu magari, unajua kabisa kwamba ili gari iwake, lazima iwe na betri yenye chaji.
Na betri za siku hizi siyo kama za zamani ambapo kila baada ya muda zinahitaji kuchajiwa.
Badala yake betri hizo zinajichaji zenyewe wakati gari inaenda.
Ndiyo maana gari isipowashwa kwa muda mrefu, hata kama betri ni nzima haitawasha kwa sababu haina chaji, kwa kuwa gari haijawashwa muda mrefu, haijapata nafasi ya kuchajiwa.
Vitu vingi kwenye maisha yetu vipo kama betri ya gari, vinachajiwa wakati vinatumika.
Chukua mfano wa mazoezi, ndiyo yanahitaji nguvu ya mwili kuyafanya, lakini unapoyafanya mwili unapata nguvu zaidi. Hivyo mazoezi ni njia ya mwili kujichaji wenyewe.
Ukienda kwenye fikra zetu pia hali ni hiyo hiyo, fikra unazokuwa nazo zinachochea kupata fikra za aina hiyo zaidi. Ruhusu fikra moja hasi na muda mfupi baadaye unajikuta umekata tamaa kabisa. Wakati ukiruhusu fikra chanya unajikuta ukiwa na matumaini zaidi.
Kadhalika kwenye fedha, kama unataka kupata fedha zaidi, lazima utumie fedha. Mfano unaweza kuwa na biashara ambayo mauzo yako chini, kwa sababu wengi hawaijui. Ili kuongeza mauzo lazima uweke fedha zaidi kwenye masoko, ambayo yatafanya watu waijue biashara na kushawishika kununua. Pesa ni chaji ya pesa zaidi, kama utajua namna bora ya kuitumia.
Kwa kuwa unajua chochote unachotaka kinajichochea mwenyewe, hakikisha kila wakati unakuwa kwenye mwendo, usisimame lwa muda mrefu mpaka chaji iishe kama gari ambayo haijawashwa muda mrefu.
Kocha.