2278; Mafanikio makubwa yanayaka usiwe wa kawaida…

Huwezi kupata mafanikio makubwa kwa kuwa mtu wa kawaida, kufanya yale wengine wanafanya kwa namna ambayo wengine wanafanya.
Yaani ulishajiona tu watu wanakuelewa, sahau kuhusu mafanikio, kwa sababu hakuna kikubwa na cha tofauti utakachokuwa unafanya.
Ili upate mafanikio makubwa, lazima ufanye kitu ambacho wengine hawawezi kufanya, na hapo ndipo unapohitaji kuwa na utofauti mkubwa na wengine.
Unahitaji utofauti kuanzia kwenye unachofanya na hata namna unavyofanya.
Eneo la kwanza na muhimu kujitofautisha ni kwenye kazi.
Watu wanaweza kukuzidi akili, wakakuzidi elimu, wakakuzidi pesa na kukuzidi ‘koneksheni’ lakini usikubali wakuzidi kwenye eneo hili moja muhumu; KAZI.
Kuwa tayari na weka juhudi kubwa kwenye kile unachofanya kuliko wengine wote.
Wakati wengine wanajipa mapumziko, wewe weka kazi, wakati wengine wanazembea na kuleta uvivu wewe weka kazi.
Lazima ujitoe sana kwenye kuweka kazi kiasi cha watu kukuambia mbona unajitesa, wakuambie maisha yako hayana mlinganyo na mengine ya aina hiyo.
Kumbuka kuna maisha ya watu wa kawaida, ambao wana muda wa kufanya mengi yasiyohusika na kazi au biashara zao. Halafu kuna maisha ya wale wanaofanikiwa sana, ambao hawana muda wa kuhangaika na yaliyo nje ya kazi au biashara zao.
Lazima uchague, iwe ni kuishi maisha ya kawaida na ukubalike na wengine lakini usipate mafanikio makubwa au uishi maisha ya tofauti, usieleweke na kukubalika na wengi ila ufanikiwe sana.
Ni moja kati ya hayo na siyo yote kwa pamoja.
Rasilimali muhimu kwetu ambazo ni muda, nguvu na umakini zina uhaba na ukomo mkubwa, zipangilie na kuzitumia vizuri kama unataka mafanikio makubwa.
Kocha.