2283; Hataki au hawezi…

Kama unampa mtu kazi ya kufanya na haifanyi vizuri, tatizo linaweza kuwa moja kati ya haya mawili.
Ni labda hataki kuifanya au hawezi kuifanya.
Ili uweze kumsaidia kufanya, lazima ujue tatizo ni hataki au hawezi.
Kujua tumia kigezo hiki, kama maisha ya mtu huyo yangetegemea yeye kufanya hicho ambacho hafanyi vizuri, je angekifanya vizuri?
Yaani kama ni asipoweza kufanya basi hana maisha, je atafanya vizuri?
Kama jibu ni ndiyo atafanya vizuri basi kinachomzuia sasa ni hataki na mtu huyo anahitaji motisha ili aweze kufanya kitu hicho vizuri.
Kama mtu hataki kufanya kitu, motisha sahihi kwake unaweza kumsukuma akifanye vizuri.
Na motisha sahihi unatemea, kuna ambaye fedha zaidi inampa motisha, mwingine sifa na kutambuliwa, mwingine uhuru wa kuamua mwenyewe na mwingine adhabu.

Kama jibu ni hapana, yaani hata kama maisha ya mtu yanategemea yeye kufanya kitu husika bado hawezi kukifanya vizuri, basi tatizo ni hajui jinsi ya kukifanya vizuri.
Na kutatua tatizo hili mtu anahitaji mafunzo, mafunzo yatakayomjengea uwezo wa kufanya kitu hicho vizuri.
Kwa kujua anapokwama, mafunzo sahihi yanaweza kumsaidia mtu akafanya kazi yake vizuri.

Tatizo la waajiri na mabosi wengi ni kutokujua tatizo la walio chini yao kushindwa kufanya vizuri na hivyo kutoa suluhisho lisilo sahihi.
Kama mtu hajui kufanya kitu, hata umpe motisha kiasi gani, bado hataweza kukifanya.
Na kama mtu hana motisha wa kufanya kitu, hata umpe mafunzo kiasi gani, hatakifanya vizuri.

Jua tatizo halisi, kama hataki apewe motisha, kama hawezi apewe mafunzo.
Na kama vyote haviwezekani, yaani ni mvivu tu na mzembe basi hafai.
Kocha.