2284; Hatari za kipumbavu…
Iko wazi kabisa kwamba huwezi kufanikiwa bila ya kuchukua hatua ambazo ni hatari.
Na hiyo ni kwa sababu hizo ni hatua ambazo wengi wanaziepuka hivyo ukizichukua unakuwa huna ushindani mkubwa.
Wapo watu kwa kusikia hivyo, hukimbilia kuchukua kila aina ya hatari, kwa sababu penye hatari ndiyo penye mafanikio.
Hatari nyingi watu wanazochukua ni za kipumbavu, kwa sababu ni hatari zinazowaumiza, hata wakipata wanachotaka.
Kila hatari unayoichukua unapaswa kuikokotoa na hesabu yako iwe kupata ni mara kumi ya unachoweza kupoteza. Lakini pia ujue kila njia unayoweza kupoteza na jinsi ya kuikabili.
Hatari unayochukua bila kukokotoa ni kamari tu na kwenye kamari, kupata au kukosa kuko nje ya uwezo wako.
Siyo kila wanachoogopa kufanya watu basi inabidi ukifanye kwa sababu wewe ni jasiri au unataka mafanikio.
Kuna sababu kwa nini watu hawakifanyi, je unaijua sababu hiyo? Je unaweza kuivuka?
Siyo kila fursa unayoona wengine hawaichangamkii basi ni fursa ya wewe kuifanyia kazi kama hatari. Kuna sababu kwa nini watu hawajaichangamkia fursa hiyo, je unazijua sababu hizo na jinsi ya kuzivuka?
Hili hutokea kila mara, mtu anafika eneo fulani na kuona kuna biashara fulani haipo, anaona ni fursa, anaikimbilia na kuishia kupoteza fedha. Yote ni kwa sababu aliparamia hatari asiyoijua.
Kwa kila fursa inayokuja kwako au unayokutana nayo, jiulize kwa nini wewe. Usidhani wewe ndiye mwenye akili sana ya kuziona fursa, au wewe ndiye jasiri sana. Kama kitu kina manufaa, watu wangeshakifanya zamani na wala usingekikuta kama fursa.
Wewe unakikuta kama fursa kwa sababu kina hatari, je umeijua na kuikokotoa hatari hiyo kabla ya kuanza?
Ipo kauli moja maarufu kwamba kama upo kwenye dili fulani na watu wengine na hujui nani ni ‘fala’ (ambaye atapoteza) kwenye dili hilo, basi wewe ndiye ‘fala’.
Usiingie kwenye hatari yoyote bila ya kuijua na kuikokotoa, utakuwa umeingia kwenye hatari ya kipumbavu na utapoteza sana.
Kocha.
Asante Sana kocha kwa maneno ya makala hii.kweli ni muhimu kuikokotoa hatari kwenye fursa kabla ya kuingia.
LikeLike
Karibu Beatus.
LikeLike