2291; Mchakato wa mafanikio…
Mafanikio ni mchakato, ambao unahitaji juhudi na muda wa kutosha mpaka uweze kuyafikia.
Mchakato huo una vipengele kadhaa, ambavyo unapaswa kuvifuata bila kuacha hata kimoja.
Kipengele cha kwanza ni kujua kile hasa unachotaka kupata au kufikia. Lazima ujue mafanikio kwako yana maana gani. Kama hujui unakotaka kufika, hutajua njia ya kukufikisha na hata ukichukua njia yoyote hutajua hata ukifika.
Kipengele cha pili ni kujaribu njia mbalimbali za kufika unakotaka kufika mpaka utakapopata njia sahihi kwako. Njia huwa ni nyingi, lakini siyo zote zinazoweza kukufaa wewe. Kujua njia sahihi kwako lazima ujaribu njia mbalimbali zinazoelekea unakotaka mpaka utakapokutana na njia sahihi kwako. Njia sahihi ni ile ambayo kwako ni burudani wakati kwa wengine ni kazi ngumu.
Kipengele cha tatu ni kufanya zaidi kile kinacholeta matokeo sahihi na kuacha kisicheta matokeo mazuri. Kila unachofanya, fanya tathmini ya matokeo unayopata kisha rudia zaidi kinacholeta matokeo mazuri.
Kipengele cha nne ni kuendelea na mchakato unaozalisha matokeo sahihi mpaka pale mchakato huo unapoacha kutoa matokeo sahihi. Watu wengi huwa wanapenda kuhangaika na vitu vipya, wanaacha vinavyowalipa sasa na kwenda kuhangaika na vipya wasivyojua kama vinalipa. Wewe usifanye kosa hilo, usiache kufanya kinacholipa na kwenda kuhangaika na usichokuwa na uhakika nacho. Endelea kufanya kinacholipa mpaka kitakapoacha kulipa.
Kipengele cha tano ni marudio, mchakato mzima unapaswa kurudiwa kadiri unavyokuwa hai. Kwa kila unachotaka, weka mchakato huo.
Leo jikumbushe vipengele hivyo vya mchakato kwenye mafanikio unayofanyia kazi sasa.
Kocha.