2297; Misimu Ya Maisha…
Kila kitu kwenye asili, huwa kinaenda kwa misimu.
Na hiyo ni kwa sababu kwenye asili hakuna kilichosimama, kila kitu kipo kwenye mwendo.
Maisha yetu pia yana misimu mbalombali, lakini wengi hatulijui hilo.
Tunachofikiri ni maisha kama safari ya njia iliyonyooka, kuanzia kuzaliwa mpaka kufa.
Lakini hivyo sivyo maisha yalivyo, safari ya maisha ni njia yenye kona nyingi, jenye kupanda na kushuka.
Japo mwanzo wa wote ni kuzaliwa na mwisho ni kufa, hapo katikati kila mtu anapitia yake.
Na hapo ndipo tunapitia misimu mbalimbali ya maisha, ambayo yote ina manufaa kwenye maisha yetu.
Unapitia misimu ambayo kwako unaona ni mizuri na misimu ambayo unaona ni mibaya.
Kuna misimu ambayo huwezi kuikwepa hata ufanye nini na ipo unayoisababisha kwa tabia zako.
Muhimu ni kujua misimu ipi iko kwenye udhibiti wako, yaani inayotokana na tabia zako na kuijenga vyema.
Na kwa misimu iliyo nje ya uwezo wako, kujiandaa kuikabili vyema.
Miti hupukutisha majani wakati wa ambao msimu siyo mzuri ili kupunguza upotevu wa maji. Na hilo linaiwezesha miti hiyo kuja kuzalisha majani zaidi wakati ambapo msimu ni mzuri.
Jua misimu ya maisha yako, kazi, biashara, mahusiano na chochote unachofanya ili uweze kuitumia misimu hiyo kwa manufaa yako zaidi.
Kutegemea maisha yaende kwenye mstari mnyoofu ni kujidanganya, hata mti unajua kuna misimu.
Hivyo acha kujidanganya na ikabili asili ilivyo.
Kocha.