2298; Kusikia unachotaka kusikia…

Mwandishi mmoja amewahi kusema, kusoma vitabu vingi vya maendeleo binafsi (personal development/self help) ni sawa na kufanya punyeto, unaweza kujisikia vizuri ila hakuna kinachobadilika kwenye maisha yako.

Hilo lina ukweli kwa sehemu kubwa kwa sababu vitabu vingi vya maendeleo binafsi na hata wahamasishaji walio wengi huwa wanawaambia watu kile wanachotaka kusikia.

Na watu wanapenda kusikia maneno mazuri, kwamba wanaweza kuwa chochote wanachotaka, kwamba wakifikiri chanya kila kitu kitakuja kwao, kwamba hakuna anayeweza kuwa kama wao.

Japo kauli hizo ni kweli kabisa, huwa hazitolewi na ukweli kamili. Huwa zinatolewa na ukweli nusu na watu hawaambiwi namna asili inavyofanya mambo yake.
Kabla hujapata chochote unachotaka, utapitia magumu mengi, utakutana na kila kikwazo.
Njia ya mafanikio siyo rahisi, mengi utakayofanya utashindwa vibaya sana.

Hivyo kama unataka kuujua ukweli juu ya jambo lolote lile, acha kutafuta kusikia kile unachotaka kusikia.
Na pale ushauri au mafunzo unayopata yanaonesha mambo ni mazuri na rahisi tu, shtuka haraka, unapewa ukweli ulio nusu.

Tunapenda kusikia mambo mazuri tu na hata matapeli hutumia hilo kuwalaghai watu, huku wakitumia mifano ya uongo ya watu walionufaika ili mtu ashawishike na kunasa kwenye mitego yao.

Kama haupo tayari kusikia usiyotaka kusikia, yanayoweza kukuumiza na kukukatisha tamaa, hujawa tayari kwa mafanikio makubwa.

Jamii ya sasa imejaa jumbe nyingi mno za kuwafurahisha watu, kuanzia kwenye habari, hadithi za mafanikio, makala, ushauri mbalimbali na hata vitabu.
Watu wameshagundua vitu vinavyowabembeleza watu ndiyo vinauza na wao wanatembea humo humo.

Lakini jua hayo yote yameandaliwa kuwalenga asilimia 99 ya watu kwenye jamii ambao hawaishi maisha yako na pia hawafikii mafanikio makubwa.
Asilimia 1 kwenye jamii huwa hawaishi kwa namna hiyo, wana maisha yao ya tofauti kabisa, wanaukabili ukweli jinsi ulivyo na kufanya kilicho sahihi.

Kila siku unayoianza una uhuru wa kuchagua kama utaishi wanavyoishi 99% au 1% na kuchagua kusikiliza yanayokufurahisha ni kujiweka moja kwa moja kwenye 99% na kujihakikishia kwamba hutafanikiwa.

Tambua kwamba asili huwa inaenda itakavyo na haifuati maoni au matakwa ya yeyote yule. Nenda hivyo na asili, kuwa tayari kupokea usiyoyataka au kuyapenda na kuyatumia kupata unachotaka.

Kocha.