2302; Jumbe Zinazokinzana…
Katika kujifunza na kupata ushauri mbalimbali, unakutana na jumbe za aina nyingi.
Kuna baadhi ya jumbe zitakuwa zinakinzana. Mmoja anakuambia kifanya kitu A ni sahihi, mwingine anakuambia kitu A siyo sahihi.
Je katika hali kama hiyo unapaswa kuchukua hatua gani?
Hapo wengi hukwama, kwa sababu hung’ang’ania jumbe zote mbili.
Sasa unajua nini kinatokea? Hawafanyi chochote, wanajikuta wamesimama.
Ni sawa na kukanyaga mafuta na breki kwa wakati mmoja kwenye gari. Gari itatumia mafuta mengi, lakini haitasogea hata hatua moja.
Ndivyo watu wanavyoendesha maisha yao, wanajifunza mambo mengi kweli kweli, lakini maisha yao hayabadiliki.
Kwa sababu jumbe wanazopata zinakinzana na wao wanang’ang’ana na zote mbili. Wakati mwingine wanaenda mbali zaidi na kutaka kutafuta ujumbe upi ni sahihi zaidi ya mwingine.
Unachopaswa kujua ni kwamba, katika jumbe zinazokinzana, zote zinaweza kuwa sahihi. Hivyo kutafuta ulio sahihi zaidi ni kupoteza muda wako.
Jumbe zote zinaweza kuwa sahihi katika muktadha tofauti.
Hivyo unapojikuta kwenye hali kama hii, jiulize unataka kupata nini au kufika wapi, kisha chukua ujumbe unaokufaa kwa wakati huo.
Usipoteze muda kujiuliza upi ni sahihi, wewe chukua unaokusaidia kwa wakati huo.
Na kadiri unavyokwenda, jenga falsafa yako ya kujifunza na chagua aina gani ya jumbe unazichukua na kufanyia kazi na zipi unajifunza tu.
Kamwe usikubali kushikilia jumbe zinazokinzana kwa wakati mmoja na kutokuchukua hatua.
Chagua ujumbe unaokufaa na fanyia kazi.
Na ili kuepuka kupoteza nguvu na muda wako, chagua aina ya jumbe unazohitaji kwenye hatua uliyopo ya safari ya maisha yako kisha fuata hizo tu. Jumbe nyingine zinazokinzana achana nazo.
Kilicho muhimu kwako ni kufika unakotaka kufika kwa njia zilizo sahihi. Ujumbe au maarifa yanayokusaidia kufika huko na ambayo hayapo kinyume na maadili au sheria ndiyo unapaswa kuyapa kipaumbele.
Kocha.