2304; Alama Tatu Za Umasikini…
Kitu kikubwa kinachowatifautisha masikini na matajiri siyo kinachoonekana, bali kisichoonekana.
Kwa maana kuwa zile sababu wengi wanafikiri ndiyo zinawatofautisha siyo, bali namna ya kufikiri ndiyo inawatofautisha.
Wanavyofikiri matajiri ni tofauti kabisa na wanavyofikiri masikini na hapo ndipo tofauti inapoanzia.
Kuna alama kubwa tatu za umasikini ambazo ni zao la fikra zao, ukiziona hizo, jua wazi hapo umasikini ndiyo nyumbani.
Alama ya kwanza ni lawama, masikini ni wazuri sana kwenye mchezo wa lawama.
Kila hali waliyonayo, wana mtu au kitu cha kulaumu kuhusika. Na kwa sababu huwa wanatafuta lawama, huwa hazikosekani.
Kwa kulalamika kwao, wanakuwa wamekiri kwamba maisha yao siyo jukumu lao na wako tayari kuathiriwa na chochote.
Alama ya pili ni kuhalalisha, hapo mtu anajifariji kwamba mambo siyo mabaya sana kwake.
Masikini hujihalalishia kwamba umasikini ni mzuri kwa kutumia kauli kama fedha siyo kila kitu, fedha hainunui furaha, matajiri ni watu wabaya n.k.
Ukisikia mtu anatoa kauli za aina hiyo, akibeza utajiri na kusifia umasikini, moja jua mtu huyo ni masikini wa kutupwa na mbili jua hawezi kutoka kwenye umasikini huo kama hatabadili fikra zake.
Alama ya tatu ni kulalamika, hapa mtu anaonesha kwamba walichofanya wengine siyo sahihi.
Masikini hupenda kulalamikia kila kitu wakati wao wenyewe hakuna hatua sahihi wanazochukua. Ni watu wanaojiona wako sahihi zaidi ya wengine na hilo linawafanya wasiwe tayari kujifunza na kupiga hatua.
Kuishia kwao kulalamika hakubadili chochote kwenye maisha yao, zaidi ya kuwaacha kwenye umasikini.
Alama hizi tatu ni kama kilevi kwa masikini, unapolaumu wengine unaona siyo wajibu wako, unapohalalisha unajiona uko pazuri na unapolalamika unajiona uko sahihi na wengine ndiyo wanaokosea.
Lakini hebu jibu swali hili, ni kiasi gani cha fedha mtu anaingiza kwa kufanya hayo matatu?
Jibu liko wazi, sifuri.
Haingizi chochote,
Ndiyo maana anabaki masikini.
Na hiyo inamaanisha mambo hayo matatu ni ya kuepuka kama ukoma kama unataka kutoka kwenye umasikini.
Kocha.