2307; Wanachokulipa ndiyo thamani yako…

Ni kawaida kuwasikia watu walioajiriwa wakilalamika kwamba waajiri wao wanawalipa mshajara kidogo, ambao hauendani kabisa na thamani yao.

Pia wapo waliojiajiri na walio kwenye biashara ambao wanalalamika kipato au faida wanayoingiza ni ndogo ukilinganisha na thamani yao.

Iko hivi rafiki, kama umeajiriwa na mwajiri wako haogopi kukupoteza, yaani hata ukiamua kuacha kazi leo hakuna anachopoteza kwa sababu ni rahisi kupata mtu wa kuziba pengo lako, basi chochote anachokulipa ni zaidi ya thamani yako.

Kadhalika kama uko kwenye biashara na kama usipofungua biashara yako kwa muda na wateja wakawa hawakutafuti, kwa sababu hakuna wanachokosa, chochote unachopata kwenye biashara hiyo ni zaidi ya thamani.

Kama unabisha haya, kama unaamini kweli una thamani zaidi ya unacholipwa sasa, nini kinakufanya ubaki hapo ulipo?
Si uondoke hapo na uende ambapo thamani yako itatambulika na kulipwa kinachostahili?

Huondoki kwa sababu ndani yako unajua wazi hakuna sehemu nyingine unaweza kulipwa unacholipwa sasa.

Na hata kama ipo, hujiamini kiasi cha kutosha kufanya maamuzi ya kutoka hapo ulipo.

Lengo la makala hii siyo kukufanya ujione huna thamani na kuendelea kubaki hapo ulipo, bali kukupa hasira ya kutoa thamani zaidi ili uwe huru kuipeleka pale ambapo watu wako tayari kuilipia kwa kadri unavyotaka wewe.

Zalisha thamani kubwa mno, thamani ambayo hakuna mwingine anayeweza kuizalisha na kisha watake watu wakulipe kile unachostahili kulipwa.

Na kama hawapo tayari au hawawezi kukulipa hivyo, ondoa thamani hiyo na peleka kwa wengine wanaoithamini na kuimudu.

Usiwalalamikie watu hawakulipi kulingana na thamani yako, anza kuangalia ni thamani kiasi gani unayo.
Kama ipo kweli, watu hawatakuwa tayari kuipoteza.

Kocha.