2309; Vitu vya kushangaza…
Waliofanikiwa wanajua kuna mengi hawajui na hivyo kuwa tayari kuendelea kujifunza kupitia kila fursa wanayoweza kuitumia.
Ambao hawajafanikiwa wanaamini wanajua kila kitu na hawana haja ya kijifunza, na hivyo hawajifunzi.
Matajiri wana fedha nyingi, lakini matumizi yao huwa siyo makubwa. Masikini hawana fedha, ila matumizi yao ni makubwa.
Walio bize huwa wanakamilisha majukumu yao kwa muda. Ambao hawapo bize, yaani walio na muda wa kutosha, huwa hawakamilishi majukumu yao kwa muda.
Wanaojua mambo kwa kina huwa siyo waongeaji sana. Wasiojua mambo kwa kina huwa ni waongeaji mno.
Matajiri hununua mali ambazo zinawazalishia zaidi baadaye. Masikini hununua mizigo ambayo inawagharimu zaidi baadaye.
Kwenye mafunzo mbalimbali, wale wasioyahitaji sana huwa ndiyo wa kwanza kuyapata. Lakini wale wanaoyahitaji sana huwa wanachelewa kuyapata.
Hapa umepata jibu kwa nini wenye nacho huongezewa na wasiokuwa nacho wananyang’anywa hata kidogo walichonacho.
Kwa sababu wenye nacho wanajua siri ya kupata zaidi huku wasiokuwa nacho wakiwa hawajui siri hiyo.
Kwa kila unalofanya, jiulize kama unajiweka upande wa wenye nacho au wasiokuwa nacho.
Usikubali kuishi maisha ya kujishangaza mwenyewe.
Kocha.