2314; Tofauti kwenye malipo ya kazi…

Bernard Russell amewahi kusema kazi ni za aina mbili.
Aina ya kwanza ni kufanya kazi husika na aina ya pili ni kuwaambia watu jinsi ya kufanya kazi husika.

Akaendelea kusema aina ya kwanza ya kazi siyo nzuri na hailipi vizuri, ila aina ya pili ya kazi ni nzuri na inalipa vizuri.

Kwa kutumia kauli hiyo ya Russell kwenye kazi, tunapata aina tatu za kazi na malipo yake.

Aina ya kwanza ni kufanya kazi husika, hii hailipi sana, lakini ndiyo inayofanywa na wengi. Wengi wanapenda aina hii ya kazi kwa sababu haina hatari na mtu anapangiwa cha kufanya. Hapa ndipo walipo wafanyakazi wote.

Aina ya pili ni kuwapangia watu kazi za kufanya, hii ina malipo mazuri kuliko wale wanaofanya na inafanywa na wachache. Aina hii ya kazi ina majukumu makubwa. Hapa ndipo walipo mameneja mbalimbali.

Aina ya tatu ni kumiliki kazi inayofanywa, hapo unakuwa umemuajiri anayewapangia watu kazi na yeye anawasimamia wale wanaofanya kazi. Kazi hii inalipa sana na inafanywa na wachache mno, ila ina hatari kubwa. Hapa ndipo walipo wajasiriamali wakubwa.

Kama hujaelewa vizuri, tupate mfano.
Kuna fundi ujenzi ambaye anafanya kazi ya kujenga hoteli.
Fundi huyo ameajiriwa na anasimamiwa na injinia ambaye anampangia kazi za kufanya.
Injinia amepewa kazi hiyo na mjasiriamali anayetaka kuwa na hoteli.
Unaona hapo mtiririko wa kazi ulivyo na hata malipo pia.

Mara zote lenga kufika ngazi ya juu kabisa, siyo kwenye kufanya kazi au kusimamia wanaofanya kazi, bali kuimiliki kazi nzima.

Kocha.