2322; Hekima mpya na upumbavu mpya…
Watu wenye hekima wa vizazi vyote wamekuwa wakisema mambo yale yale.
Na hayo ndiyo mambo sahihi ambaye yeyote akiyazingatia anakuwa na maisha bora.
Hakuna hekima mpya ni zile zile ila zinaboreshwa kuendana na kizazi husika.
Kujijua wewe mwenyewe, kuishi kusudi la maisha yako, kuwatendea wengine kama ambavyo ungependa wakutendee, kutoa thamani kubwa kwa wengine, kuwa mnyenyekevu na kujifunza endelevu siyo vitu vipya.
Vimekuwa vinashauriwa tangu enzi na enzi, lakini bado wapo wengi ambao wanachagua kutokuvielewa.
Wapumbavu wa miaka yote wamekuwa wakifanya kinyume na yale yanayofanywa na wenye hekima.
Wapumbavu wamekuwa wakirudia makosa yale yale ambayo yamekuwa yanafanywa na wapumbavu tangu enzi na enzi.
Hakuna upumbavu mpya, bali unabadilika kuendana na zama husika.
Kuishi maisha yasiyo na kusudi, kuendekeza tamaa za mwili, kiburi, majivuno, ujuaji, ulaghai, ubinafsi na ulafi ni vitu ambavyo vimekuwepo miaka na miaka na vimekuwa chanzo cha matatizo mengi.
Pamoja na ushahidi uliopo, unaoonesha jinsi wapumbavu wa kale walivyokosea na kuadhibiwa vibaya kwa yale waliyofanya, bado wapumbavu wa sasa wanayarudia hayo hayo. Watapata walichopata wenzao na bado hawatajifunza.
Hivyo ndivyo dunia imekuwa inakwenda na ndivyo itakavyoendelea kwenda. Wenye hekima wataishi kwa misingi ya hekima huku wapumbavu wakiishi kwa misingi ya upumbavu.
Hakuna ajali au bahati mbaya kwenye maisha, kila kinachotokea kimesababishwa, iwe mtu anajua au hajui.
Unapojua jinsi unasababisha maisha yako na ukachagua kusimama kwenye misingi ya hekima, lazima uwe na maisha bora.
Huhitaji kugundua hekima mpya au upumbavu mpya, tayari vipo, ni wewe kuvifuata tu.
Kocha.