2334; Ushujaa Siyo Kupambana Pekee…
Watu wengi hudhani ili wawe mashujaa lazima wapambane kwenye kila linalowakabili.
Lakini ushujaa siyo kupambana pekee, wakati mwingine kuepuka mapambano ni njia sahihi na yenye manufaa kwako.
Sun-Tzu aliyekuwa mwandishi wa kivita wa China ya kale na aliyeandika kitabu cha Art of War alishauri unaposhambuliwa ukiwa hujajiandaa usijibu mashambulizi, badala yake kimbia.
Lengo lako ni kushinda vita kuu na siyo kushinda kila aina ya pambano. Kwa kuepuka baadhi ya mapambano, unakusanya nguvu zako kuweza kushinda vita kuu.
Hii ni mbinu ya kivita ambayo unaweza kuitumia kila siku na ukayafanya maisha yako kuwa bora na kuweza kufanikiwa.
Baadhi ya maeneo unayoweza kutumia mbinu hii ni kama;
- Siyo lazima umjibu kila anayekupinga au kukukosoa, wengine waache wakihangaika na hayo ili upate nafasi ya kufanya makubwa zaidi.
Kumbuka aliyechagua kukupinga na kukukosoa hiyo ndiyo kazi yake kuu, hivyo hata ukijitetea atatafuta udhaifu kwenye utetezi wako na kuzidi kukupinga.
Wakati mwingine waache waongee ili wakuache ufanye yako. -
Siyo lazima umwangushe kila mshindani wako kwenye safari ya mafanikio ndiyo uweze kufikia mafanikio makubwa.
Unatakiwa uwaache washindani wako kwani wanasaidia kulikuza soko.
Na wewe unapaswa kutoa huduma bora sana na kuangalia madhaifu yao kisha kuboresha kwako kiasi kwamba wateja wanapokuwa na malalamiko kwake wanakuja kwako. -
Kwenye mahusiano siyo lazima kila wakati uwe sahihi. Wakati mwingine kubaliana tu na watu hata kwa yasiyo sahihi ili tu kupunguza misuguano isiyo na lazima. Wakubalie upande wao ndiyo sahihi, hasa pale ambapo kukubali hakukupelekei kufanya usichokubaliana nacho.
Labda ni ubishani unao na mtu mwingine na anasema kitu fulani ndiyo bora wakati wewe unajua kingine ndiyo bora, kubaliana naye tu ili mmalize hilo.
Utulivu na maelewano ni bora kuliko kuwa sahihi.
Unaweza kulazimisha upande wako ndiyo sahihi halafu ukapoteza ushirikiano na upande wa pili. -
Kukabiliana na changamoto kubwa na ambayo hukutegemea, ikaishia kukuangusha siyo mwisho wa safari. Jipange kwa wakati mwingine kufanya kwa ubora.
-
Ukikutana na wezi wenye silaha huku wewe huna silaha yoyote au huwezi kutumia silaha yako dhidi yao, wape wanachotaka wakuache ukiwa salama. Kuliko kujaribu kuonesha ushujaa, ukapoteza unachokataa nacho na ukaumizwa pia.
Kumbuka katika mikakati yako muhimu ya mafanikio, moja wapo ni kuhakikisha unakuwa hai, salama na kwenye mapambano mpaka utakapokutana na bahati yako.
Shujaa siyo yule aliyepigana kwenye kila pambano, ila aliyeweza kubaki kwenye mapambano kwa muda mrefu zaidi.
Tumia kila mbinu kuhakikisha unabaki kwenye mapambano kwa muda mrefu zaidi.
Kocha.