2337; Adui Mkuu Kwenye Vita Ya Maisha Yako…
Maisha ni vita na adui mkuu unayepambana naye ni muda.
Japo mwisho adui huyo atashinda, kwa kuwa utakufa, ushindi wako ni jinsi utakavyokuwa umetumia muda wako ukiwa hai.
Nguvu kuu ya adui huyo ni msimamo, haangalii wewe unafanya nini, yeye anafanya yake na kukuvuta zaidi kwenye kaburi lako.
Kama kuna vitu unasubiri unaweza kusubiri utakavyo, lakini jua muda hautasubiri na wewe, utaendelea kupungua na wewe kupoteza fursa za kufanya mengi zaidi.
Kila siku inayoisha ni ushindi kwa adui muda, je ni ushindi gani unaoweza kuhesabu kwako kwa kila siku inayoisha?
Siku ambayo umetumia kufuatilia habari, mitandao ya kijamii na maisha ya wengine ni siku ambayo umeshindwa.
Siku ambayo umetumia kujiboresha zaidi na kupiga hatua za ziada kwenye kile unachofanya ni siku ya ushindi.
Kila mwisho wa siku alama zinawekwa, kwa adui muda na kwako. Kwa kuwa adui muda hapotezi, kwa kuwa masaa 24 ya kila siku anayatafuna, ni wajibu wako kuhakikisha kila ndani ya masaa 24 kuna kitu unafanya ambacho unakihesabu ni ushindi.
Soma, andika, ongea na wateja zaidi, boresha kazi au biashara, washawishi watu wa kushirikiana nao, zione fursa mpya na jinsi ya kuzitumia.
Fanya kila namna ili siku iwe ya ushindi mkubwa kwako.
Kusudi la maisha yako ni kuishi maisha yenye kusudi.
Na maisha yenye kusudi ni unapokwenda kulala ukijua umefanya kila kilichopaswa kufanyika kwa siku hiyo, umefunga vitabu vya siku, hakuna chochote ulichoahirisha au kupeleka mbele.
Imalize kila siku kwa ushindi, kama vile ndiyo siku ya mwisho kwako kuwa hapa duniani. Kama utapata siku nyingine iwe ni ya nyongeza nayo uitumie vizuri pia.
Hapo juu nimekuambia kwamba mwisho wa hii vita muda utashinda, lakini wapo wachache wanaoushinda muda.
Lengo kuu la muda kwenye hii vita ni kukuondoa hapa duniani na kufuta kumbukumbu zako zote.
Lakini wachache wamekuwa wanashinda, licha ya kuondoka duniani, kumbukumbu zao zinabaki kwa muda mrefu.
Hilo pia linaweza kukutokea kama utaishi kila siku kwa ushindi mkubwa.
Siku ya ushindi ni ile ambayo umeweka juhudi zako zote, umecheka, umejali, umependa na umefanya maisha ya mwingine kuwa bora zaidi ya yalivyokuwa awali.
Hayo yote yako ndani ya uwezo wako kama utaacha kuhangaika na usumbufu, ukasikiliza nafsi yako na kuyaishi maisha yako.
Kumbuka adui muda hajali chochote kuhusu wewe bali kufanya yake.
Hivyo pia ndivyo unapaswa kuwa, usijali chochote nje ya kuyaishi maisha yako kwa ushindi.
Shinda kila siku ili kujenga maisha ya ushindi.
Kocha.