2339; Mlango Wa Sita Wa Hisia…

Tumeizoea milango mitano ya fahamu.
Macho yanayoona.
Masikio yanayosikia.
Pua inayonusa.
Ulimi unaoonja.
Ngozi inayohisi.
Milango hiyo mitano ndiyo tunayotumia kuwasiliana na dunia ya nje.

Upo mlango wa sita wa fahamu ambao wengi hawaujui.
Mlango huo siyo wa kuwasiliana na dunia ya nje, bali wa kuwasiliana na wewe mwenyewe.

Mlango wa sita wa fahamu ni nafsi yako, sauti ndogo iliyo ndani yako ambayo huwa inakuambia mambo mbalimbali ila huwa unaipuuza.

Mlango huu wa fahamu unajua mengi mno kuhusu wewe kwa sababu umekusanya taarifa na uzoefu wote ambao umewahi kuwa nao tangu unazaliwa mpaka sasa.

Mlango huo wa fahamu unakuambia vitu ambavyo akili yako haiwezi kuvithibitisha, na ndiyo maana ni rahisi kupuuza yale ambayo sauti hiyo inakuambia.

Jifunze kutumia mlango wako wa sita wa fahamu, tenga muda wa kukaa peke yako na kuisikiliza nafsi yako, kusikia kile sauti ya ndani inakuambia.

Kwa kusikiliza sauti ya ndani na kuhusisha akili yako kwenye kuchakata taarifa ulizonazo, utaweza kufanya maamuzi bora kabisa kwako.

Unapokuwa unafanya maamuzi yoyote makubwa kwenye maisha yako, kuna sauti huwa inasema na wewe, kamwe usiipuuze, ni mlango wa sita wa fahamu ambao unayajua mengi uliyosahau.

Kocha.