2340; Ukomavu Wa Kiroho…
Kama kuna kitu muhimu unachohitaji kwenye hii safari ya mafanikio basi ni ukomavu wa kiroho.
Unapoianza safari hii ya mafanikio unakuwa mchanga kiroho, unakuwa na msukumo mkubwa wa kubadili maisha yako na kutaka kila anayekuzunguka abadilike mara moja.
Utawalazimisha wabadilike na utawashangaa pale ambapo hawaelewi unachowashawishi.
Utabishana nao na kuwapinga wazi wazi pale wanapoamini, kusema au kufanya kitu unachojua ni tofauti kabisa na misingi ya mafanikio.
Lakini utakachokipata kwenye hilo ni maumivu na hali ya kutokuelewana na wale wote wanaokuzunguka, wewe utawaona wa ajabu na wasiofaa, na wao watakuona hivyo pia.
Uliweza kukua kiroho na kufikia ukomavu, unagundua jinsi hayo yote uliyokuwa unafanya yalivyokuwa ubatili kwa sababu hayajamsaidia yeyote.
Hapo ndipo unapojifunza kuenda na watu kama walivyo, unapojifunza kwamba hata utake kiasi gani, huwezi kumbadili yeyote kwenye maisha kama hajaridhia kubadilika.
Hapa unakuwa tayari kukubaliana na watu hata kama wanakosea, kwa sababu unajua hiyo ndiyo njia rahisi kwako kupata muda na nguvu ya kufanya yale yaliyo sahihi kwako.
Ukomavu wa kiroho ni pale unapomkubalia mtu kwamba 2 + 2 = 5 kwa sababu ndivyo ameamini kwa maisha yake yote.
Hukubaliani naye kwa sababu ndiyo jibu sahihi, jibu sahihi unalijua, ila unakubaliana naye kwa sababu huna muda na nguvu za kupoteza. Maana hata uoneshe uthibitisho kiasi gani, bado watabaki kwenye kile wanachoamini.
Ukomavu wa kiroho ni kuweza kutambua pale watu wanapokuwa na imani na itikadi kali na kutokuhangaika kuwapinga kwenye hilo kwa namna yoyote ile.
Wasio na ukomavu wa kiroho wataona kufanya hivyo ni udhaifu na kutokuwa tayari kusimama kwenye ukweli.
Lakini unapokuwa na ukomavu wa kiroho unajua watu wakiwa na imani na itikadi kali hawajihusishi na ukweli bali uhalisia na uhalisia ni kile wanachoona wao.
Kama wanachoamini wengine hakiingilii kwa namna yoyote mambo yako unayofanya, basi huna haja ya kuhangaika kupinga imani zao.
Na kama wanachoamini kinaingilia mambo yako, waoneshe mpaka wao unaishia wapi na hapo mtaweza kushirikiana vizuri.
Kocha.