2341; Visingizio ni vingi, sababu ni moja…
Muulize mtu yeyote kwa nini hajaanza kuziishi ndoto kubwa alizonazo na majibu huwa ni yale yale kwa wato wote;
Sina muda, nimebanwa sana.
Sina fedha, kipato hakitoshi.
Sina ujuzi, sikupata elimu sahihi.
Sina ‘koneksheni’, sijazungukwa na watu sahihi.
Majibu hayo yanaweza kuonekana kama ni sababu za kweli ambazo zina mashiko.
Lakini sivyo, hasa ukizingatia zinatumika na kila mtu na zinajirudia miaka na miaka.
Chukua mfano wa mtu anayesema kila siku anataka aanzishe biashara ila hana mtaji, mwaka huu anasema hana mtaji, na miaka mitano iliyopita pia alisema hana mtaji. Unafikiri mtaji ni sababu ya kweli?
Au chukua mfano wa mtu anayesema hana muda wa kufanya juhudi za ziada ili aweze kuishi ndoto zake, lakini mtu huyo huyo yupo kwenye mitandao ya kijamii, anajua kila habari inayoendelea na ni shabiki wa michezo mbalimbali. Unaamini muda ni sababu ya kweli?
Mifano ipo mingi, ila kwa hiyo miwili utajionea wazi kile ambacho watu wanaita sababu za kukwama siyo sababu kweli, bali ni visingizio tu.
Sababu ya kweli kabisa ya kwa nini mtu hajaanza kuishi ndoto zake ni moja tu, HANA UJASIRI WA KUTOSHA.
Kuishi ndoto zako siyo lele mama, lazima uwe na ujasiri mkubwa wa kuachana na visingizio na kukabiliana na uhalisia ambao siyo rahisi.
Lazima uweze kuwakabili wengi wanaokurudisha nyuma au wanaokuzuia usipige hatua.
Ukiwa na ujasiri wa kutosha hakuna kinachoweza kukuzuia kuishi ndoto zako. Ukiwa huna ujasiri wa kutosha, kila kisingizio kitaonekana ni sababu kubwa.
Jijengee ujasiri huo mkubwa ili uweze kupambana na chochote kinachokukabili katika kuziishi ndoto zako.
Kocha.
Asante Sana kocha , nahitaji ujasiri wa kukabili uhalisia ambao siyo rahisi ili kuishi ndoto yangu. Tupo pamoja.
LikeLike
Vizuri Tumaini.
LikeLike