2346; Kabla Hujabishana…

Wengi hupenda kubishana lakini ubishani wao huwa hauna manufaa yoyote kwao.
Kwani huwa wanashindwa kuwashawishi wale wanaobishana nao.

Huwa nashauri sana watu kuachana na ubishani wa aina yoyote ile.
Lakini kuna nyakati ubishani haukwepeki, hasa pale unapotaka kusimamia kile kilicho sahihi.

Lipo sharti moja muhimu unalopaswa kutimiza kabla hujaingia kwenye ubishani wowote ule.
Sharti hilo ni kuhakikisha unaweza kuelezea vizuri upande wa pili kuliko wanavyoweza kujielezea wao wenyewe.

Yaani uweze kutetea ule upande unaoshindana nao vizuri kuliko upande huo unavyojielezea wenyewe.

Ukiweza kufanya hivyo, utakuwa umeelewa vizuri kwa nini upande huo unaamini vile unavyoamini.

Hilo litapeleka ufanye moja kati ya haya mawili,
Moja ni kutokubishana nao kwa sababu umeshaelewa wanasimama wapi.
Mbili ni kubishana nao kwa ushawishi sahihi wa pale wanaposimama.

Wengi hukimbilia kubishana bila hata kuelewa upande wao vizuri, kinachotokea ni kelele ambazo hazimsaidii yeyote.

Uelewe upande wako vizuri na elewa upande wa pili vizuri kuliko upande huo unavyojielewa wenyewe na kama kwa kufanya hivyo bado utaona umuhimu wa kuendelea na ubishani basi utakuwa wenye manufaa.

Kocha.