2354; Ng’ang’ana na lengo, siyo njia…
Kitu muhimu kabisa na unachopaswa kung’ang’ana nacho kwenye maisha yako ni malengo makubwa uliyonayo.
Piga, ua garagaza, hakikisha unapambana kwa kila namna kuyafikia malengo hayo makubwa.
Lakini hupaswi kung’ang’ana na njia moja katika kuyafikia malengo yako.
Njia zipo nyingi, kuna ambazo ni sahihi na ambazo siyo sahihi.
Kazi yako ni kujifanyia tathmini kwa kila njia uliyotumia na kuona kama inakufikisha kwenye lengo au la.
Kama alivyowahi kusema Albert Einstein, ujinga ni kufanya jambo lile lile, kwa njia ile ile ila kutegemea matokeo ya tofauti.
Kama unatumia njia fulani ambayo haikufikishi kwenye lengo, lakini unaendelea kung’ang’ana nayo, tatizo siyo njia, tatizo ni wewe.
Gharama ambazo tumeshaweka kwenye njia tunayotumia huwa zinatuzuia kuachana na njia hiyo na kwenda kwenye nyingine.
Lazima uwe tayari kusahau gharama hizo ili uweze kwenda kwenye njia sahihi.
Njia ni nyingi, lakini siyo zote ni sahihi kwako. Hupaswi kung’ang’ana na njia moja tu uliyochagua. Ng’ang’ana na lengo na tumia njia mbalimbali mpaka upate ile sahihi kwako kufika kwenye lengo.
Kocha.