2355; Utapiamlo Wa Akili…

Watu wengi hasa kwenye zama hizi wana utapiamlo wa akili.
Kama ilivyo kwamba usipoulisha mwili vizuri unapata utapiamlo wa mwili, ndivyo pia usipoilisha akili vizuri unapata utapiamlo wa akili.

Ili kuondokana na utapiamlo wa akili, unapaswa kuilisha akili yako kilicho sahihi. Unapaswa kuwa na dayati maalumu kwa ajili ya akili yako ambayo itagusa maeneo haya matatu.

Moja ni kujua chakula sahihi cha akili. Hapa ni kuchagua maarifa na taarifa sahihi za kulisha akili yako ambazo zinachangia kufika kule unakotaka kufika.

Mbili ni kuondoa vyakula vyote vichafu kwa akili. Hapa unaachana kabisa na taarifa na maarifa hasi ambayo hayana manufaa kwako.

Tatu ni kujenga na kuimarisha umakini wako kwenye kile unachofanya kwa wakati husika. Kuhakikisha fikra zako zote zipo kwenye kile unachofanya badala ya kuziacha tu zizurure hovyo.

Maarifa na taarifa zisizo sahihi kwa akili yako huwa zina sifa ya kuwa zinazogusa sana hisia na kujenga hali ya utegemezi, kuona usipofuatilia unapitwa.
Maarifa na taarifa hizo hazina manufaa yoyote kwa mtu zaidi ya kumchosha na kumwacha akiwa na hisia kali za wivu, chuki au hasira.

Usikubali akili yako iwe ndiyo jalala la kukusanya kila aina ya uchafu. Iweke safi na libda usafi huo usivurugwe na chochote.

Kocha.