2356; Usisubiri Yapoe…

Kitu pekee ambacho nimekuwa nanufaika nacho kwenye maarifa mbalimbali ninayopata ni kujiuliza nawezaje kuyatumia na kisha kuchukua hatua mara moja, kabla hata maarifa hayo hayajapoa.

Huduma zote ambazo nimeweza kuanzisha na kuboresha mpaka sasa ni kutokana na utaratibu huu wa kuyatumia maarifa yakiwa ya moto badala ya kusubiri mpaka yapoe.

Hata chakula huwa ni cha moto pale unapokula kikiwa ni cha moto, kikishapoa hata ladha huipati.

Tumia utaratibu huu kwako pia, unapojifunza kitu kipya au wazo jipya linapokuja kwako, swali la kwanza kujiuliza linapaswa kuwa ni unawezaje kutumia hayo.

Na ukishaona njia ya kutumia, basi chukua hatua mara moja kabla maarifa hayo au wazo hilo halijapoa.

Siyo yote utakayoanza kwa namna hiyo yataendelea na kuzaa matunda makubwa, lakini kadiri unavyofanya kwa wingi, ndivyo utakavyokutana na mawazo mazuri na yakakunufaisha sana.

Usisubiri mpaka yapoe, yafanyie kazi yakiwa bado ni ya moto moto.

Kocha.