2357; Jiweke kwenye fikra zao…
Mtu akikuambia nitakutafuta, usisubiri mpaka akutafute, utakuwa umechagua kumpoteza.
Hasa pale wewe ndiye unayekuwa unahitaji zaidi kitu kutoka kwake.
Ipo kauli inayosema kisichoonekana huwa kinasahaulika.
Kadhalika kwa wale wanaokuambia watakutafuta, ni rahisi kusahau kama hakuna kinachowafanya wakukumbuke.
Na hapo ndipo unapaswa kujiweka kwenye fikra zako, ili wasikusahau na waweze kukutafuta kama walivyokuahidi.
Njia nzuri ya kujiweka kwenye fikra za watu ni kuwa na mawasiliano nao ya mara kwa mara.
Na siyo mawasiliano ya kuwakumbusha walichoahidi, bali mawasiliano ya kawaida kabisa.
Mfano kuwasalimia au kuwatakia heri kwenye mambo mbalimbali.
Pia unaweza kuwatumia mapendekezo mazuri uliyokutana nayo ambayo yanaweza kuwa na manufaa kwao.
Kila siku, jiulize ni fursa ipi unayo ya kuwasiliana na wale ambao hutaki wakusahau, kisha tumia kila fursa unayopata.
Muhimu ni uhakikishe mawasiliano yako hayawi usumbufu kwao, bali yanakuwa sehemu ya kuongeza thamani zaidi kwao.
Watu wana mambo mengi, watu wamevurugwa na usumbufu unaowazunguka. Kama walikuahidi watakutafuta halafu hawajafanya hivyo, kosa siyo lao, bali kosa ni lako wewe. Umewapa nafasi ya kukusahau.
Kuwa na mkakati wa kuhakikisha wote waliokuahidi vitu wanakukumbuka. Na mawasiliano ya mara kwa mara ndiyo yanaweza kukusaidia kwenye hilo.
Kocha.