2363; Hiyo siyo kazi yao…

Unataka kila mtu akubaliane na wewe ndiyo ufanye kile unachotaka, unajichelewesha bure.

Unataka kila mtu akupende ndiyo uone umekamilika, utasubiri sana.

Unataka watu wakuheshimu ndiyo ujione una thamani, utazidi kujipoteza.

Siyo kazi ya wengine kukupenda, kukukubali na kukuheshimu, hiyo ni kazi yako mwenyewe.

Kinachowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa ni katika kuchukua wajibu huo.

Wanaofaniwa hawasubiri wengine wawapende, kuwakubali au kuwaheshimu. Wanajipa hayo wao wenyewe na wengine wanakuwa hawana namna bali kuenda nao hivyo.

Wanaofanikiwa wao hutaka kwanza wengine wawapende, wawakubali na kuwaheshimu ndiyo nao wajichukulie hivyo. Huhangaika kufanya mambo kuwafurahisha wengine, lakini bado hawapati kile wanachotaka kwao.

Usifuate njia ya wanaoshindwa, chagua kuyaishi maisha yako, jipende, jikubali na jiheshimu. Simamia hilo bila ya kutetereka kwa namna yoyote ile. Wengine hawatakuwa na namna bali kukuchukulia hivyo.
Huwaombi, ni maisha unayokuwa umechagua na wao hawana budi bali kwenda na wewe kwa namna hiyo.

Maoni ya wengine yasikuyumbishe kwa namna yoyote ile, kama unachofanya ni sahihi na chenye manufaa, waache wengine wawe na maoni wanayotaka.

Kumbuka hata uchague kufanya nini, kuna watu watakuwa na maoni mazuri na wengine maoni mabaya kuhusu wewe.
Hakuna chochote utafanya na watu wote wakakukubali, hakipo kabisa.

Usitake kuwapa wengine wajibu ambao umekushinda wewe.
Usilalamike mbona wengine hawakuheshimu, jiulize wewe unajiheshimuje.
Usiseme wengine hawakupendi, wewe mwenyewe unajipenda?

Shika wajibu wa maisha yako, na wengine watakuchukulia kwa namna unayojichukulia mwenyewe.
Usikimbie wajibu wako halafu uje kulaumu wengine.

Kocha.