2364; Jifunze, Nufaika, Fundisha…

Kusudi kuu la maisha ya viumbe wote hapa duniani ni kuzaliana.
Na siyo tu kuzaliana, bali kuzaliana kwa namna ambayo ni bora kabisa.

Hivi ndivyo mageuzi yamekuwa yanatokea duniani, viumbe hai wanayakabili mazingira, wanabadilika kulingana na mazingira hayo na kisha kuzaa viumbe hai walio bora zaidi kwa kuyakabili mazingira ya aiba hiyo.

Viumbe wanaoshindwa kubadilika na kuyakabili mazingira, wanakufa na hivyo kushindwa kuzalisha viumbe hai wengine.

Kusudi la kuzalisha haliishii tu kwenye watoto, bali linapaswa kwenda kwenye kila eneo la maisha.
Kwa kila unachonufaika nacho, kizalishe zaidi kwa wengine.

Umepata fedha, zalisha fedha zaidi kwa wengine ili nao wanufaike.
Ukipata maarifa, zalisha maarifa zaidi ili wengine nao wanufaike.

Msingi wako kwenye maisha unapaswa kuwa kujifunza, kisha kuyatumia uliyojifunza ili unufaike zaidi na baadaye kurudisha kwenye jamii kwa kuwafundisha yale uliyojifunza na kufanyia kazi.

Siyo wote watakaoelewa au kupokea yale unayotoa, ila wapo wachache ambao wataelewa na kunufaika pia.

Kwa kila unachojifunza, jiulize unakwenda kukitumiaje kwenye maisha yako ili kiwe na manufaa. Panga kabisa lini unaanza kukifanyia kazi na fanya kama ulivyopanga.

Unapofanyia kazi kile ulichojifunza, angalia ni changamoto zipi unazokabiliana nazo na zitatue kwa namna sahihi. Jua kila unachopitia na matokeo unayoyapata.

Baada ya kuchukua hatua na kunufaika, andaa maarifa na uzoefu ulioupata na washirikishe wengine.
Na hata kama umefanyia kazi maarifa na hukunufaika, ripoti pia, utawasaidia wengine wasirudie makosa kama yako.

Kitu pekee ambacho kimeiwezesha sayansi kukua sana ni hili la mtu kuripoti matokeo aliyopata, yawe ni mazuri au mabaya.
Kila mwanasayansi anayefanya jaribio lolote lile, anaripoti hatua zote alizopitia na matokeo aliyopata. Haijalishi ni mazuri au mabaya.
Kwa kufanya hivyo, anawasaidia wanasayansi wengine kujua wapi wanaanzia na wasirudie makosa kama yake.

Jifunze, Nufaika, Fundisha ni msingi rahisi ambao ukiuishi, utaacha alama kubwa hapa duniani, hata kama hujazalisha matokeo makubwa sana.

Kocha.