2366; Mtu Sahihi Wa Kusikiliza Ukosoaji Wake Kwako…

Kitu chochote kile utakachofanya kwenye maisha yako, kuna watu watakukosoa.
Watu watachagua kuwa na maoni kuhusu wewe kwa namna wanavyotaka wao wenyewe na siyo unavyotaka wewe.

Ukisema umsikilize kila mtu au kutaka kumridhisha kila mtu, hutaweza kufanya kitu chochote kikubwa kwenye maisha yako.

Lakini pia ukisema usisikilize ukosoaji wa yeyote, hutaweza kupata mtejesho wa kile unachofanya ili uweze kuboresha zaidi.
Huwa ni vigumu kuona udhaifu au makosa yako mwenyewe.

Hivyo unapaswa kujua watu sahihi ambao unaweza kusikiliza ukosoaji wao na kujifunza ili uweze kuboresha zaidi kile unachofanya.

Mtu sahihi kwako kusikiliza ukosoaji wake ni yule ambaye pia unaweza kuchukua ushauri wake.
Kwa maana nyingine, usichukue ukosoaji kwa mtu ambaye huwezi kuchukua ushauri kwake.

Mtu anayeweza kukupa maoni yatakayoweza kukusaidia ni yule ambaye anaelewa kwa kina kile unachofanya.
Maoni ni rahisi kutoa, lakini yaliyo sahihi siyo rahisi.

Hivyo ukimpata yule anayeelewa kweli unachofanya na akakupa maoni, yasikilize, hata kama yanakuumiza.
Kuna kitu anakiona ambacho wewe mwenyewe huwezi kukiona kwako.

Kwa chochote unachofanya, jitahidi upate watu wanaokielewa kweli na walio tayari kukupa mrejesho wa kweli hata kama unakuumiza.

Watu wengi wanaokujali hawapo tayari kukuumiza, hivyo wanaweza kujua kabisa unapotea, lakini wakakuacha tu, kwa sababu hawataki kukuumiza.

Wale wasiokujali wanachoangalia ni jinsi ya kukuumiza tu, hawajali kama kitu ni sahihi au la.

Kupata anayekujali na aliye tayari kukupa mrejesho wa kweli hata kama unakuumiza, ni kupata hazina kubwa itakayokuwezesha kufanya makubwa.

Tafuta watu wa aina hii na kama huwezi kuwapata basi watengeneze. Watakusaidia kuona kile ambacho kwako ni upofu.

Kocha.