2368; Uhuru Siyo Rahisi…

Watu huwa wanapenda kuzungumzia uhuru, kueleza jinsi wanavyotaka kuwa na uhuru zaidi kwenye maisha yao.

Lakini ukweli ni kwamba, uhuru siyo rahisi.
Kwanza siyo rahisi kuupata.
Na pili siyo rahisi kuutunza.

Kuupata uhuru ni vigumu kwa sababu hakuna atakayekuwa tayari kukuacha uwe huru, unahitaji kupambana kweli kweli na kuchukua uhuru wako.

Lazima udhihirishe wazi kwamba unaweza kusimama mwenyewe na kukabiliana na lolote linalokuja kwako ndiyo watu waweze kukuacha uwe huru.

Lakini pia kutunza uhuru baada ya kuupata ni zoezi jingine ambalo ni gumu zaidi.
Uhuru haimaanishi ufanye vile unavyojisikia wewe.
Bali uhuru unahitaji uwe na nidhamu kali juu yako mwenyewe.
Uweze kupanga na kusimamia mambo yako.
Na pia uweze kujiadhibu wewe mwenyewe, bila ya kujionea huruma

Wengi hawapo huru kwenye maisha yao kwa sababu kubwa mbili.

Moja ni hawapo tayari kupambana kupata uhuru wao. Wanaona ni bora tu kufuata mkumbo na kutokusumbuliwa kwa kuwa tofauti.

Mbili ni hawana nidhamu binafsi ya kujisimamia wenyewe na kujiadhibu pale inapostahili. Hivyo wanaona ni bora wawape wengine nafasi hiyo ya kuwasimamia na kuwaadhibu.

Unafikiri kwa nini mtu kwenye kazi ya kuajiriwa anaweza kuwahi kila siku ila kwenye biashara yake binafsi hawezi kuwahi?
Ni kwa sababu hawezi kutumia uhuru, hivyo ameamua awaachie wengine.

Wengi huharibu maisha yao baada ya kuwa huru, kitu kinachowafanya wapoteze uhuru ambao waliupata kwa muda.

Pambania uhuru kama kweli una nidhamu ya kutosha kuutunza uhuru unaopata, la sivyo uhuru huo utayavuruga maisha yako kabisa.

Uhuru na ukweli ni kama moto, ukiutumia vizuri una manufaa, ukiutumia vibaya unaunguza.

Ipo kauli inayosema mafanikio makubwa yanakuja na wajibu mkubwa.
Kadhalika kwenye uhuru, kadiri uhuru wako unavyokuwa mkubwa ndivyo nidhamu ya kuulinda inavyopaswa kuwa kubwa pia.

Kocha.