2369; Mambo Yanayoathiri Maamuzi Unayofanya…

Sehemu kubwa ya maamuzi unayofanya kwenye maisha yako, siyo maamuzi yako binafsi.
Japo unaweza kujiambia umeyafanya mwenyewe, kuna vitu vingi vinavyoathiri maamuzi yako na kukushawishi ufanye maamuzi ya aina fulani.

Maamuzi yoyote unayofanya ukiwa kwenye kundi kubwa la watu, ni tofauti kabisa na yale unayofanya ukiwa peke yako.
Ndiyo maana watu wanaotaka ushawishike kwa namna fulani, hawatakuruhusu ufanye maamuzi peke yako, bali watahakikisha unayafanya ukiwa kwenye kundi.

Maamuzi unayofanya baada ya kusikia habari, matangazo au kutembelea mitandao ya kijamii pia siyo maamuzi yako. Njia hizo zinaathiriwa sana na propaganda mbalimbali. Na propaganda huwa zinakuwa na nguvu, kwa sababu hazimpi mtu nafasi ya kufikiria yeye mwenyewe.
Unapigwa na wimbi la taarifa nyingi, zote zikiwa na lengo la kukushawishi kwa namna fulani.

Na kitu cha juu zaidi ni itikadi, mtu akishabeba itikadi fulani, inaathiri maamuzi yake yote anayoyafanya.
Itikadi ni imani kali ambayo mtu anakuwa nayo kuhusu kitu fulani na ambayo hayumbishwi kwa namna yoyote ile. Mtu anakuwa mnazi kwenye kitu hicho na hafikirii kwa namna yoyote ile, anapokea kitu kama kilivyo.

Kama unataka kufanya maamuzi bora kabisa kwako, hakikisha hakuna athari za vitu hivyo hapo.
Hakikisha haupo kwenye kundi ambalo linakushawishi kwenye maamuzi hayo, pia epuka propaganda ambazo zinaenezwa kwa njia mbalimbali.

Kuepuka kundi unaweza kutenga muda wa kuwa peke yako, kujihoji maswali na kujipa majibu, hilo ni rahisi kwako.
Ni muhimu sana uwe unatenga muda wa kuwa peke yako.

Kuepuka propaganda epuka kila chombo cha habari, iwr tv, redio, magazeti au mitandao, na pia epuka mitandao ya kijamii.
Hili linaweza kuonekana gumu kwenye zama zetu lakini linawezekana.

Ugumu upo kwenye itikadi, maana hicho ni kitu kinachoathiri kabisa saikolojia yako, kitu kinachojenga nafsi yako.
Unahitaji ujikane wewe mwenyewe, uue sehemu ya nafsi yako na uzaliwe upya.
Ni kitu kigumu na kinachohitaji jitihada kubwa.

Mara nyingi mtu huwa hujijui kama itikadi inakuathiri, ni kama samaki aliye kwenye maji, hana uelewa sana kama yuko kwenye maji, yeye anaona ni maisha yake ya kawaida.

Kufanya maamuzi sahihi, hasa kwa zama tunazoishi sasa ni kitu kigumu mno.
Sehemu kubwa ya watu hawafanyi maamuzi, wanajiendea tu kwa kufuata mkumbo. Hawa ni watu wanaopelekwa kama bendera.
Wachache mno ndiyo wanaofanya maamuzi na ndiyo wanaopata kile wanachotaka, maana wanashawishi wengine wakubaliane na maamuzi yao, waone kama ni maamuzi yao binafsi.

Tunaamini kila changamoto ni fursa, na katika hili la maamuzi, kuna fursa kubwa mno ukiweza kufanya maamuzi yako mwenyewe bila ya kuyumbishwa na yeyote.
Umeshajifunza hapa jinsi ya kuondokana na ushawishi mbaya kimaamuzi, chukua hatua.

Kocha.