2375; Ni Mapendekezo, Siyo Amri…
Mawazo mengi yanayokuja kwenye akili yako huwa ni mapendekezo na siyo amri. Ni maoni na siyo ukweli.
Akili yako ni kiwanda cha kuchakata mawazo ya kila aina. Na huwa yanabadilika kulingana na hali na mazingira yanavyobadilika.
Mfano unaweza kuwa umepanga jukumu muhimu la kufanya, lakini wakati unataka kuanza kufanya, ukaanza kupata mawazo kwamba unahitaji kupangilia vitu fulani kwanza, au kuwasiliana na mtu kwanza, au kuingia mtandaoni kwanza.
Ni rahisi kusikiliza mapendekezo hayo na kuona ni vitu muhimu kufanya kabla ya kile ulichopanga.
Lakini kama tulivyoona, hayo ni mapendekezo, siyo lazima uyasikilize.
Una nguvu ya kuachana nayo na kufanya kile ulichopanga kufanya kama ulivyopanga.
Na unapoamua kuendelea kufanya, akili yako inabadilika na kukuletea mapendekezo mengine.
Ukiweza kudhibiti fikra zako na kubaki kwenye kile ulichoamua, akili haiwezi kukuyumbisha.
Ila kama utashindwa kudhibiti fikra zako, utakuwa unafuata kila mapendekezo ya akili yako na hutaweza kufanya makubwa.
Akili zetu huwa hazipendi kufanya mambo magumu, hivyo unapokikabili chochote kigumu, itakuletea mapendekezo ya vitu vingine ambavyo ni rahisi zaidi.
Unajua kwa nini ni vigumu mtu kusoma kitabu lakini rahisi kuperuzi mtandao au kuangalia tv? Kwa sababu akili inakupa mapendekezo zaidi unapofanya vitu vigumu kuliko ukiwa unafanya vitu rahisi.
Usitii kila fikra zinazokuja kwenye akili yako, siyo sheria, ni mapendekezo tu na mengi lengo lake ni utoroke kwenye kile unachofanya.
Lakini pia ni rahisi kusikiliza mapendekezo hayo unapokuwa umechoka, hivyo unapokuwa na magumu ya kufanya au kuamua, yafanye wakati hujachoka.
Fikra zako siyo amri, ni mapendekezo. Una nguvu ya kuchagua yapi ya kufuata na yapi ya kupotezea. Muhimu ni uweze kufanya kile unachopanga kufanya.
Kocha.