Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye KISIMA CHA MAARIFA, kuna vitu vitatu ambavyo kila mwanachama anapaswa kuvijua kuhusu yeye na kuviishi kwenye kila siku yake.

Kwa kuvijua vitu hivyo vitatu, mtu hawezi kubaki kwenye maisha ya kawaida, lazima atapiga hatua kubwa sana kutoka pale alipo sasa.
Vitu hivyo vitatu ndiyo nguzo muhimu za kuyajenga mafanikio ya kila mtu.

Kitu cha kwanza ni mtu kujua kusudi la maisha yake, kujua yuko hapa duniani kufanya nini.
Kusudi la maisha ndiyo injini inayoendesha maisha ya kila mtu. Ndiyo kitu kinachokusukuma uendelee kuchukua hatua bila ya kukata tamaa hata pale mambo yanapokuwa magumu.

Wengi wanaohangaika kwenye maisha na hawafanikiwi, huhitaji kuanzia mbali, wewe waulize tu swali moja, nini kusudi la maisha yako? Utaona jinsi wanababaika, hawawezi kukuambia mara moja, kwa sababu hawajui. Na kinachofanya wahangaike kwenye maisha ni kwa sababu hawajalijua hasa kusudi la maisha yao

Rafiki yangu, kama na wewe  bado hujalijua kusudi la maisha yako, leo una bahati kubwa, kwani nakwenda kukupa kusudi leo leo na uanze kulifanyia kazi.
Kuanzia leo, kusudi la maisha yako ni kujua kusudi la maisha yako.
Anzia hapo na ninakuhakikishia utalijua kusudi na utakapolijua tu, maisha yako yatabadilika sana.

Ninakuambia kwa uhakika kwa sababu kwenye KISIMA CHA MAARIFA nimeanza na wengi ambao hawakuwa wanajua kusudi, ila nilipowaapa kusudi hilo haijachukua muda wengi tayari wameshajua kusudi la maisha yao.

Ushuhuda wa aliyeanza akiwa hajui kusudi la maisha yake, ila baada ya kumpa kusudi la kujua kusudi, haijamchukua muda amelijua kusudi lake. Wewe unasubiri nini?

Kitu cha pili unachohitaji ni kuwa na ndoto kubwa za maisha yako.
Kama hujafanikiwa na unaishi maisha ya kawaida tu, ni kwa sababu huna ndoto kubwa zinazokusukuma.

Kama unafanya kazi au biashara yako kwa mazoea, unafanya kama wengine wanavyofanya na hujisukumi kwa namna ya ziada ni kwa sababu malengo uliyonayo ni madogo sana.

Kama unapoteza muda kuzurura kwenye mitandao, kufuatilia habari na maisha ya wengine, kulewa na kufanya starehe za kila aina, ni kwa sababu hakuna malengo makubwa yanayokusumbua na kukuweka juu juu muda wote.

Ndani yako una uwezo wa kufanya makubwa sana, lakini uwezo huo hautaweza kutumika kama huna ndoto kubwa unazopambana kila siku kuzifikia.

Unapaswa kuwa na ndoto kubwa mno, ambazo mtu yeyote akisikia unazisema anashtuka na kukuambia haiwezekani. Ila wewe unakuwa na picha kamili ya ndoto hizo huku ukiwa na mpango unaofanyia kazi kila siku ili kuzifikia.

Kwenye KISIMA CHA MAARIFA hili ni hitaji jingine muhimu mno, lazima uwe na ndoto kubwa ambazo kila siku unapambana kuzifikia. Kila siku unajikumbusha ndoto hizo na kuchukua hatua kuzifikia.
Kitendo tu cha kujua na kuona kabisa wapi unakwenda, kina nguvu kubwa ya kukubadili sana namna unayaishi maisha yako.

Nimewahi kusema na hapa narudia tena, hakuna mtu mvivu duniani, bali wapo watu ambao hawajajua kusudi la maisha yao na hawana ndoto zozote kubwa. Ukitaka kuthibitisha hilo, mchukue yeyote unayeona ni mvivu kabisa, mpeleke kwenye kina kirefu cha maji kisha mzamishe kwa nguvu.
Utashangaa jinsi atakavyokuwa na nguvu ya kutoka kwenye maji unayomzamisha.
Kwa sababu hapo ana kusudi moja tu, kuendelea kuwa hai.

Kulijua kusudi lako na kuwa na ndoto kubwa ni mahitaji muhimu sana kwa mafanikio ya mtu yeyote yule.

Mwenzetu aliyeanza akiwa hajui kusudi lake ni lipi, lakini baada ya kupata mwongozo sahihi, akaweza kujisikiliza na kutambua kile kilicho ndani yake hasa. Karibu na wewe upate mwongozo utakaokusaidia.

Kitu cha tatu ni utambulisho wako.
Kikwazo kikubwa mno kwa wengi kufanikiwa ni namna wanavyojitambulisha kwao binafsi na kwa wengine pia.
Utambulisho wako una nguvu kubwa mno, kwani huwezi kukua zaidi ya utambulisho huo.

Utambulisho wako ni matokeo ya hadithi unayoiamini na kuiishi kwenye maisha yako. Kila kinachotokea kwenye maisha yako utakilazimisha kiendane na hadithi na utambulisho wako.
Hiyo ni kwa sababu akili yako haipendi ukinzani, hivyo inarahisisha kila kitu kiendane na hadithi unayoiishi.

Hapa kuna manufaa makubwa, ina maana kwamba, ukitengeneza hadithi yako mpya na ukawa na utambulisho mpya, utayalazimisha maisha yako yaendane na hadithi na utambulisho mpya ulionao.

Chukua hatua mara moja hapa, jitambulishe kwa neno moja tu ambalo linabeba vile unavyotaka kuwa, kisha tengeneza hadithi ya kuhalalisha neno hilo kwako.
Unaweza kujitambulisha kama mjasiriamali, au mwekezaji, au mpambanaji, au mbishi au mwalimu.
Wewe angalia kusudi ulilonalo na ndoto kubwa unazotaka kufikia, kisha jipe utambulisho unaobeba hayo na uishi utambulisho huo kila siku.

Jitambulishe kama mtu ambaye tayari ameshakuwa na siyo kujiambia nitakuwa. Usijiambie nitakuwa mjasiriamali, bali jiambie mimi ni mjasiriamali.
Ukishajitambulisha, jipe hadithi inayoelezea utambulisho huo. Kama umejitambulisha ni mjasiriamali, jua wajasiriamali huwa wanafanya nini. Ili unapojiita mjasiriamali, ulazimike kufanya wanachofanya wajasiriamali.

Kama tulivyoona, akili haipendi ukinzani, ukishajitambulisha upya na kuwa na hadithi mpya, akili itakulazimisha maisha yako yaende kwa namna hiyo mpya. Pale utakapokuwa unafanya kile ambacho ni kinyume na utambulisho na hadithi yako mpya, hitajisikia vizuri na hilo litakurudisha kwenye mstari.

Jitambulishe upya na jenga hadithi inayotetea utambulisho wako mpya na ishi hivyo kila siku. Kwa kufanya hivyo utayaona maisha yako yakibadilika na kuendana na upya wako.

Mwenzetu aliyeweza kufanya mabadiliko makubwa kwenye maisha yake baada ya kuwa kwenye programu maalumu. Unadhani maisha yako yameshindikana? Njoo tufanye kazi pamoja, utayaona mabadiliko makubwa kwako.

Kazi yangu kubwa kwako.
Rafiki, katika haya matatu niliyoshirikisha hapa, siyo tu nakuhubiria wewe uhangaike nayo, bali ndiyo ninayoyaishi kila siku ya maisha yangu.

Kusudi la maisha yangu ni kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi kupitia kile ninachofanya.
Nimejipa wajibu mkubwa kwamba kila anayekutana na mimi, aondoke akiwa bora kuliko alivyokuwa awali.
Na hilo ndiyo linanisukuma kwenye kila ninachofanya.

Ndoto kubwa za maisha yangu ni mbili; kuwa Bilionea na kuwa raisi wa Tanzania. Hizi ni ndoto ambazo kila siku najiona nikiwa nimezifikia na zinaniweka kwenye njia sahihi. Maana kabla sijafanya chochote najiuliza kinachangiaje mimi kuwa bilionea au raisi wa Tanzania.

Utambulisho wangu ni Kocha. Kama Kocha ninawafundiasha, kuwaongoza na kuwahamasisha wengine kuchukua hatua sahihi ili maisha yao yawe bora zaidi. Mwalimu anafundisha na kuondoka, kocha anafundisha na kufuatilia kwa karibu, kumjua mtu kwa undani, uimara na madhaifu yake na kumshauri namna bora ya kutumia hayo ili kupiga hatua zaidi.

Kwa kila fursa ninayoipata kufanya kazi na mtu, najitahidi sana kuhakikisha anajenga mtazamo sahihi na kuchukua hatua zenye manufaa kwake. Kwangu mimi ukiniambia umejifunza mazuri kupitia kazi zangu nitakuambia sawa, lakini sitakuamini sana. Ila ukinionesha yale uliyofanya kutokana na uliyojifunza kwangu, hapo nakuamini na nafurahi pia.

Ushirikiano ninaouomba kutoka kwako.
Mimi kama Kocha, ninaomba ushirikiano wako katika kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Kitu kikubwa ninachohitaji kutoka kwako ni utayari wa kujifunza na kuchukua hatua.
Siyo tu kujifunza na kufurahia uliyojifunza, wengi wanafanya hivyo lakini maisha yao yanabaki vile vile.
Ninachotaka kwako ni uwe tayari kujifunza na kuchukua hatua kwenye yale uliyojifunza.
Haitakuwa rahisi kwa sababu mengi yatakuwa mapya kwako, na hapo ndipo ninapokuwa tayari kuambatana na wewe kwa karibu mpaka ukamilishe kile unachotaka kufikia.

Karibu sana tufanye kazi pamoja.
Kama tayari upo kwenye KISIMA CHA MAARIFA, fanyia kazi ile miongozo yote ninayoshirikisha, jibu yale ninayokuuliza mara kwa mara, unaweza kuyaona ni madogo, ila mimi kocha wako najua nguvu yake.
Kuwa tayari kuyafanyia kazi na ninakuhakikishia hutabaki pale ulipo sasa.

Kama bado hujawa kwenye KISIMA CHA MAARIFA unapoyapoteza maisha yako. Unahangaika na mengi ambayo hayana tija kwako na unakosa mwongozo sahihi kwako kufika kwenye mafanikio makubwa.
Kama kweli unataka kufikia mafanikio makubwa kabisa kwenye maisha yako, kuna sehemu moja unayopaswa kuwa, ambayo ni KISIMA CHA MAARIFA.
Amua sasa kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA au amua kuendelea na majaribio ya kupoteza maisha yako.
Kama umechoka kuyapoteza maisha yako na upo tayari kwa mafanikio makubwa, wasiliana nami sasa kwa wasap namna 0717 396 253.

Ombi la mwisho kwako rafiki yangu, naomba uwatumie marafiki zako wa karibu ujumbe huu. Watumie moja kwa moja. Mambo haya matatu niliyoshirikisha hapa, yana msaada mkubwa kwa yeyote atakayeyafanyia kazi. Fanya hivyo sasa na kuna ambao watajifunza kitu na kuyafanya maisha yao kuwa bora zaidi.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.