2381; Ubahili ulio sahihi…
Siri ya utajiri ni ubahili, hiyo iko wazi na inajulikana na wengi.
Lakini ubahili umekuwa unachukuliwa kwa mtazamo hasi, kama kujinyima na kuyafanya maisha kuwa magumu.
Ubahili ni kuhakikisha matumizi yako hayazidi kipato chako.
Na zipo njia za kuufanya ubahili kwa usahihi, ambapo maisha yako yatakwenda vizuri tu.
Ubahili siyo kujitesa, bali kuweka vipaumbele vyako kwa usahihi. Kujua kipi unapasea kukipa nafasi kabla ya kingine.
Ubahili siyo kununua vitu vya bei rahisi, bali kununua vitu bora ambavyo utakaa navyo kwa muda mrefu. Unaweza kununua kwa bei rahisi lakini ikakugharimu sana kwenye kuhakikisha kiko sawa au kupata kingine kwa sababu hakijadumu.
Ubahili ulio sahihi ni kujua tofauti ya matakwa na mahitaji. Mahitaji ni yale ya msingi kabisa, ambayo yanapaswa kutimizwa ili maisha yaweze kwenda.
Matakwa ni yale yasiyo ya msingi, ni anasa tu ambazo hata usipozipata maisha hayaathiriki.
Wengi hudhani kuwa huru kifedha ni kuweza kupata kile unachotaka kwa wakati wowote unaotaka. Lakini hebu jiulize ni nguo ngapi unazohitaji? Ni magari mangapi ya kutemvelea unayohitaji?
Ni mapumziko na starehe kiasi gani unazohitaji?
Ukiwa mfuatiliaji wa matangazo mbalimbali, kila wakati utajiona hujakamilika, kila wakati utaona maisha yako yana mapungufu.
Huo ndiyo udhaifu wa kisaikolojia ambao watangazaji wa bidhaa mbalimbali wamekuwa wanautumia kukusukuma ununue bidhaa zao. Ukiamini kwa kufanya hivyo utakuwa umekamilika, lakini bado.
Ubahili sahihi ni kujua kabisa kwamba tayari ndani yako umekamilika, huhitaji kununua chochote ndiyo uwe umekamilika.
Na kuyajua mahitaji yako ya msingi na kuhakikisha unaweza kuyamudu hayo ili maisha yako yaende vizuri.
Ubahili ulio sahihi ni kutokujilinganisha au kujifananisha na yeyote. Unanunua kitu kwa sababu una matumizi nacho muhimu na siyo kwa sababu umeona wengine nao wakinunua.
Wengi wanapopata fedha huwa haikai, kwa sababu hawana ubahili ulio sahihi.
Na wale wenye ubahili usio sahihi huteseka maisha yao yote na kufa huku wakiwaachia wengine fedha na mali ambazo wanazitumia vibaya.
Ubahili ni muhimu, lakini pia maisha yako ni muhimu zaidi, lazima yawe ambayo ni bora, yanayokusukuma kuendelea kufanikiwa zaidi.
Mahitaji yako ya msingi hakikisha unayapata. Kama huwezi kuyapata, hakuna maana kwako kutafuta utajiri.
Kocha.