Rafiki yangu mpendwa,
Moja ya hitaji muhimu la kuwa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA ni kuwa na biashara.
Naamini kila mtu anapaswa kuwa na biashara, bila kujali anafanya nini au ana kipato kiasi gani.

Ninaamini biashara ndiyo darasa kuu la maisha, ambalo litakusukuma kujifunza na kuwa bora zaidi kila siku kama unataka ufanikiwe.

Hakuna kitu kigumu hapa duniani kama kumshawishi mtu akupe fedha zake alizozipata kwa taabu. Hivyo lazima uwe unatoa thamani anayoihitaji kuliko anavyozihitaji fedha zake, lazima uamini kweli kwenye kile unachouza na lazima uwe na mbinu za ushawishi.

Biashara ya aina yoyote ile ni ngumu. Ni ngumu kwa sababu inabidi utoe thamani ambayo mteja anaihitaji kweli. Lakini ugumu unaongezwa na ushindani uliopo kwenye kila aina ya biashara.

Ili kuendesha na kukuza biashara yako katika mazingira hayo ya ugumu, lazima uwe na mpango unaoufanyia kazi. Biashara nyingi zinazoshindwa, huwa zinaendeshwa kwa mazoea, unakuta hakuna mpango wowote unaofanyiwa kazi ambao unaweza kuleta matokeo ya tofauti.

Kwa kuwa kwenye KISIMA CHA MAARIFA unafanyia kazi mafanikio yako, unahitaji kufanyia kazi ukuaji wa biashara yako. Kwani hiyo ndiyo mlango usio na ukomo kwako kufika kwenye mafanikio makubwa.

Kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2021 ambayo itafanyika tarehe 16 na 17 Oktoba 2021, nitakaa na kila mshiriki wa semina ana kwa ana na kikubwa tutakachofanya kwenye mazungumzo hayo ni kupitia mpango wa biashara wa mwaka wa mafanikio unaofuata.

Hivyo wakati unajiandaa kuja kwenye semina, andaa mpango wako wa biashara kwa mwaka wa mafanikio 2021/2022 ambao tutakaa pamoja tuupitie na kisha nikusimamie kwenye utekelezaji wake kwa mwaka mzima.

Mpango wako wa biashara kwa mwaka wa mafanikio 2021/2022 uguse maeneo haya muhimu;

1. Mfumo wa biashara.
Hapa panga ni namna gani unapunguza utegemezi wa biashara kwako, yaani biashara iweze kujiendesha hata kama haupo kwenye biashara.
Mfumo wa biashara ni eneo muhimu ambalo tutapata mafunzo ya kuutengeneza kwenye semina hii.

2. Kukuza mtaji.
Panga pia unakwenda kukuza mtaji kwa kiasi gani kwa mwaka wa mafanikio. Iwe ni kwa kukuza biashara iliyopo sasa au kuanzisha biashara nyingine kama tawi la biashara ya sasa au biashara mpya kabisa.
Hapa unapaswa kuwa na mpango kamili wa namna utakavyokuza mtaji, kama ni kwa kudunduliza faida, kutumia akiba zako au kupata mkopo kutoka vyanzo vingine.

3. Masoko.
Unapaswa kuwa na mkakati wa masoko ambao utakuwezesha kuwafikia wateja sahihi wa biashara yako na kuwashawishi kuja kwenye biashara.
Hupaswi kusubiri wateja waje wenyewe, unapaswa kuwafuata kule walipo.
Hapa pangilia kabisa njia za kuwafikia wateja na idadi ya kufikia. Kuwa na mpango mzuri wa kuwasiliana na wateja kwa njia mbalimbali.

4. Mauzo.
Wateja wanaweza kufika kwenye biashara lakini wasinunue. Lazima uwe na mkakati mzuri wa mauzo ambao unamshawishi mteja kununua anapofika kwenye biashara.
Pia uweze kumfanya mteja anunue zaidi ya alichofuata na arudi tena kununua.
Hapa utahitaji kupanga ofa zote unazoweza kutoa na kuwasukuma wateja kununua zaidi.

5. Mzunguko wa fedha.
Hii ndiyo damu ya biashara hivyo lazima uipe umakini kwani isipokaa sawa biashara inakufa.
Hapa unahitaji kuanza na mauzo ambayo ndiyo njia ya fedha kuja kwenye biashara. Panga ni mauzo kiasi gani unataka kufikia.
Jua pia gharama za kuendesha biashara yako na jinsi ya kuzidhibiti zisikue.
Na muhimu, jua kiasi cha faida unachohitaji kutengeneza kwa mwaka wa mafanikio na kisha upambane kukifikia.
Mzunguko wa fedha ukikaa vizuri, biashara inakwenda vizuri.

6. Huduma bora kwa wateja.
Hapa unahitaji kuwa na mpango wa kuwapa wateja wako huduma bora kabisa ili waendelee kununua kwako.
Unahitaji kujua wazi ni kipi cha kipekee ambacho wateja wanapata kwako na hawawezi kupata sehemu nyingine.
Unapaswa kumfanya mteja kuwa kipaumbele cha kwanza kwenye biashara yako, kila unachofanya unamuangalia mteja kwanza.
Pia unahitaji kuwa na mpango wa kuwa na mawasiliano endelevu na wateja wako, ili wawe sehemu ya biashara yako na waendelee kununua kwako.

7. Ushindani.
Mpango wako wa biashara pia unapaswa kueleza jinsi gani unajipanga kukabiliana na ushindani.
Kila biashara ina ushindani, hata kama umeanza kwa ubunifu wa kipekee, watu wakiona unapata faida wataiga biashara yako na huna cha kufanya kuwazuia wasifanye hivyo.
Njia sahihi ya kukabiliana na ushindani siyo kushindana, bali kulitawala soko ulilopo.
Hivyo unahitaji kuwa na mpango wa namna gani unakwenda kulitawala soko ulilopo.
Na kama soko limetawanyika sana na huwezi kulitawala, basi kuwa na mpango wa kutengeneza soko jipya ambapo wewe utakuwa wa kipekee na kutawala.

Rafiki, hayo ni maeneo saba muhimu sana ambayo ukiyawekea mipango na kuitekeleza kwa mwaka mzima, chini ya usimamizi wangu wa karibu, lazima utapiga hatua kubwa.

Hatua za kuchukua.
1. Kama bado hujathibitisha kushiriki SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2021 fanya hivyo sasa kwa kutuma ujumbe kwenda namba 0717 396 253 unaosema NITASHIRIKI SEMINA 2021.
2. Anza kutengeneza mpango wako wa biashara kwenye maeneo hayo saba na mengine ya nyongeza kadiri unavyopanga kukua kwenye biashara yako. Ukikwama popote  nijulishe ili tusaidiane na utengeneze mpango bora.
3. Chapa mpango wako kwa nakala mbili, moja itakuwa yako na nyingine itakuwa yangu ambayo nitatumia kukufuatilia kwa mwaka mzima wa mafanikio 2021/2022.
4. Kama bado hujaanza biashara, basi andaa mpango wa biashara utakayoanza na huo tutaanza nao pamoja, uweze kuanza biashara na kuiendesha vizuri.

Nakusubiri kwa shauku kubwa rafiki yangu kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2021 ambapo tutakaa ana kwa ana na kupitia mpango wako wa biashara kwa mwaka wa mafanikio 2021/2022.
Karibu sana utumie nafasi hii ha kipekee kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.
www.bit.ly/semina2021