2387; Juhudi ni zile zile…
Kama umeajiriwa na unaingia kazini saa moja asubuhi na kutoka saa kumi jioni, huo ndiyo muda utakaotumia kwenye kazi kila siku.
Iwe utafanya kazi nzuri au la, haijalishi, muda ni ule ule na juhudi ni zile zile.
Kadhalika kama una biashara na unafunga saa moja asubuhi na kufunga saa moja usiku, muda ni huo huo na kazi ni hiyo hiyo iwe utawahudumia wateja wako vizuri au la.
Kama umeoa au kuolewa, muda na nguvu utakazoweka kwa mke au mume wako ni zile zile iwe mtakuwa na maisha ya upendo na maelewano au mavurugano.
Kama muda na nguvu ni zile zile, kwa nini usichague kuziwekeza vyema?
Badala ya kupoteza kwa yasiyo sahihi, ziweke kwa yaliyo sahihi.
Badala ya kufanya kwa ukawaida na hovyo, kwa nini usifanye kwa upekee na ubora?
Ukimjibu vibaya mteja haifupishi siku yako ya kazi, bali inaweza kuifanya kuwa ndefu zaidi, kwa nini usimjibu vizuri na ukapata manufaa zaidi.
Jikumbushe hili kila unapoingia kwenye kazi au biashara yako, jiambie niko hapa kwa masaa kadhaa pekee, nitayatumia masaa haya kuyafanya maisha ya kila anayekutana na mimi kuwa bora zaidi.
Kwa kufanya kazi yako kwa mtazamo huu, utakuwa umewekeza vizuri muda wako na nguvu zako na hilo litakuletea matokeo bora sana.
Kocha.