Rafiki yangu mpendwa,

Katika kila biashara 10 zinazoanzishwa, 8 hufa ndani ya miaka mitano.

Takwimu hizo zinatisha, ulimwengu wa biashara ni kama vita, mapambano ni makali na hakuba hutuma.
Ni aliye imara pekee anayeweza kuvuka hatari hizo na kufanikiwa.

Sasa kwa kuwa wengi huingia kwenye biashara wakiwa hawajajiandaa, kwa kuwa wengi huanza biashara kwa sababu wameona wengine wanafanya na inawalipa, wanakuw akitoweo kizuri kwenye ushindani wa biashara.

Sababu za biashara kushindwa huwa ni nyingi, zipo zinazoanzia ndani ya biashara na zinazotoka nje ya biashara.
Lakini vipo viashiria vikuu viwili ambavyo huanza kujionyesha mapema kabisa kama biashara inaenda kushindwa.

Wengi huwa hawavioni viashiria hivi na kuchukua hatua ya haraka, huwa wanakuja kushtuka wakati mambo yameshaharibika kiasi kwamba hakuna cha kuokoa tena.

Mfanyabiashara makini, anayeijua na kuifuatilia biashara yake kwa ukaribu, anaweza kuziona dalili za biashara kushindwa mapema na kuchukua hatua sahihi ili kuiokoa.

Hapa unakwenda kujifunza viashiria viwili muhimu kuviangalia kwenye biashara ili kuepuka isishindwe.

Kiashiria cha kwanza; marejesho hasi (negative returns).

Kuna juhudi huwa unaweka kwenye biashara yako na zikazaa matunda mazuri.
Hapo unajifunza kwamba juhudi hizo ni nzuri na hivyo unaendelea kuweka juhudi hizo.

Kwa kuwa mwanzo juhudi zilileta matokeo mazuri, unajiamini na huzifuatilii tena, unaona zitaendelea kuleta matokeo mazuri

Usichojua ni kwamba kila juhudi inayoleta matokeo mazuri mwanzoni, huwa matokeo yanaenda yakipungua (diminishing return) na baadaye yanakuwa hasi kabisa (negative return).

Marejesho hasi ni pale juhudi unazoweka zinapoleta hasara badala ya faida. Juhudi unazipoteza kwenye kitu ambacho hakina manufaa tena wakati ungeweza kuziweka kwenye kitu chenye manufaa.

Mfano ni ufanyaji wa masoko, unaweza kupata njia nzuri ya kufanya masoko ambayo unapoijaribu inaleta wateja wengi zaidi.
Unaona hiyo ndiyo yenyewe, unaendelea kuitumia, ukiamini itaendelea kuleta matokeo mazuri.

Lakini kadiri muda unavyokwenda njia hiyo haileti tena wateja wengi kama awali. Hivyo juhudi unazoweka unakuwa umezipoteza.

Kuepuka hili la marejesho hasi, fuatilia biashara yako kwa umakini na pima matokeo ya kila juhudi unayoweka.
Usifanye tu kwa mazoea, badala yake pima kila unachofanya.

Angalia ni matokeo gani yanayopatikana kwa juhudi unazoweka na pale unapoona yanapungua, boresha zaidi. Usisubiri mpaka mambo yawe mabovu ndiyo uanze kuhangaika.
Ukiwa mfuatiliani na mpimaji wa biashara yako, utaona wazi wapi matokeo yanapungua na hivyo kuchukua hatua sahihi.

Kiashiria cha pili; uwekezaji uliozama (sunk cost).

Hii ndiyo yenye changamoto kubwa na ngumu zaidi kujua na kuondokana nayo.

Kuna uwekezaji ambao unakuwa umefanya kwenye biashara yako, ukitegemea uzalishe matokeo mazuri.
Lakini matokeo yanakuwa tofauti kabisa na mategemeo.

Sasa kwa kuwa umeshawekeza, unaona hutaki kupoteza uwekezaji ambao ulishafanya, hivyo unaendelea kuwekeza zaidi, kwa lengo la kuokoa uwekezaji wa mwazo.

Kinachotokea ni kadiri unavyowekeza, ndivyo unavyozidi kuzamisha zaidi na zaidi.
Unawekeza sana, lakini hakuna unachovuna kwa sababu kila unachowekeza kinazama.

Chukua mfano wa uwekezaji unaokuwa umeweka kwenye njia fulani ya masoko, lakini njia hiyo haileti matokeo mazuri.
Kwa kuwa umeshawekeza, unaona unahitaji kuwekeza zaidi kwenye njia hiyo, kitu kinachoendelea kuzamisha uwekezaji unaofanya.

Kuepuka hali hii isiathiri biashara yako fuatilia kwa kina na kwa karibu biashara yako na pima kila uwekezaji unaofanya.
Kama uwekezaji haujazalisha matokeo unayotaka, usikimbilie kwanza kuongeza uwekezaji zaidi, bali jiulize kwanza kama uwekezaji huo ni sahihi.

Mara nyingi utagundua uwekezaji siyo sahihi na hapo unapaswa kukubali kupoteza uwekezaji ambao tayari umeshaufanya.
Hapo ndipo pagumu, maana watu hawapo tayari kukubali kupoteza, hivyo wanakazana kuokoa walichowekeza kwa kupoteza uwekezaji zaidi.

Unapaswa kuwa imara mno kufanya maamuzi ya kukubali kupoteza uwekezaji ambao tayari umeshafanya ili usiendelee kuzamisha uwekezaji wako zaidi.

Viashiria hivi viwili ulivyojifunza hapa, ukivifanyia kazi, biashara yako itakwenda vizuri. Kila juhudi utakazoweka zitaleta matunda mazuri na kila uwekezaji unaofanya utalipa na kama haulipi hutasita kuusitisha.

Kujifunza zaidi jinsi ya kuendesha biashara yako kwa mtindo wa kisasa, kitu kitakachokupa uhuru na mafanikio makubwa, pata na usome kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA.
Jipatie nakala yako ya kitabu leo kwa kuwasiliana na 0752 977 170.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani.
http://www.somavitabu.co.tz