2388; Kwa nini ushauri mwingi wa mafanikio haufanyi kazi…
Vitabu vilivyoandikwa kuhusu siri za mafanikio ni vingi sana.
Hadithi za watu waliofanikiwa ni nyingi.
Na mafunzo pamoja na ushauri wa mafanikio vimejaa kila kona.
Lakini cha kushangaza, idadi ya wanaofanikiwa inabaki kuwa ni ndogo sana.
Sababu kubwa ni moja, mafunzo na ushauri mwingi kuhusu mafanikio unakusukuma uwe mtu wa aina fulani, tofauti na vile ambavyo tayari upo.
Hakuna aliyewahi kufikia mafanikio makubwa kwa kujaribu kuwa mtu wa aina ya tofauti na alivyo.
Wote waliofanikiwa sana kwanza walijitambua na kisha wakachagua kuwa wao. Wakaleta hapa duniani ule upekee wao, ambao hakuna mwingine anayeweza kuushinda.
Hakuna mtu anaweza kukushinda wewe kwa kuwa wewe. Hivyo unapojitambua na kuchagua kuwa wewe, unakuwa kwenye fursa ya kufanya makubwa.
Je kwa maana hii mafunzo na hadithi za mafanikio havina maana?
Jibu ni hapana, vina maana sana.
Ila tu vinapaswa kukuwezesha kujitambua na kuwa wewe na siyo kutaka kuwa mtu wa aina fulani, tofauti na vile ambavyo upo.
Kila mtu ameshachukuliwa, umebaki wewe tu. Jichague, jitambue, jikubali na jiamini kisha pambana kufanya makubwa.
Kingine muhimu ni kujali wengine wanakuchukuliaje.
Wasiofanikiwa wanajali sana wengine wanawachukuliaje.
Kila wanachofanya wanaangalia wengine wanakikubalije.
Sasa kwa kuwa walio wengi hawaelewi mambo ya tofauti, wanakuwa hawakubaliani nao na hilo linawakatisha tamaa wasiofanikiwa.
Wanaofanikiwa wako tofuati kwenye hilo, hawajali sana wengine wanawachukuliaje au kuwakubalije, wanachojali ni kufanya kilicho sahihi.
Wengi waligoma kupanda treni ya kwanza kwa kuamini kasi ya treni itasababisha moyo usimame.
Wengi waliamini hakuna chombo cha kutengenezwa kinaweza kuruka hewani
Wengi waliamini sauti ya mtu haiwezi kusafirishwa kwa njia ya mawimbi.
Orodha ni ndefu, ila picha umeipata.
Kwa kila unachokiona leo, kuna kipindi watu waliamini siyo sahihi au hakiwezekani.
Ni wabishi wachache waliokomaa na vitu hivyo na leo vina manufaa kwako.
Je wewe ni wapi ambapo unalibishia kundi kubwa la watu?
Kama hakuna, basi jua unachofanya ni cha kawaida na hakina nafasi ya kukufikisha kwenye mafanikio makubwa.
Unachotaka ni kufanikiwa na siyo kujua tu kuhusu mafanikio.
Chagua unaposimama ili kufanikiwa.
Kocha.