2391; Kutaka kupenda na kila mtu…

Hakuna maisha magumu hapa duniani kama kutaka kila mtu akupende.

Ni maisha magumu kwa sababu hata ujaribu kwa namna gani, huwezi kufanikiwa.

Haijalishi unafanya nini, kuna watu wanachagua tu kukuchukia.

Na hata kama unachofanya ni kizuri na chenye manufaa, bado wapo ambao hawatapenda namna unavyofanya.

Wapo watakaoona wanajua namna sahihi ya kufanya kuliko wewe na ukiwakatalia watakuchukia.

Uzuri ni kwamba, wapo watakaokupenda na kukujali kwa namna ulivyo na kile unachofanya.

Huwa tunayaona maisha ni magumu kwa sababu tunahangaika na watu wasio sahihi, wakati walio sahihi ni wengi.

Ili kupunguza ugumu na changamoto za maisha, kwanza kuwa mkweli kwako mwenyewe.

Pili fanya kila unachofanya kwa nia njema, ukiangalia namna wengine wananufaika na kile unachofanya.

Kisha wajue watu sahihi na hangaika na hao tu. Muda na nguvu zako wekeza kwa wale walio sahihi na siyo kuhangaika na wasio sahihi.

Ukiweza kuwahudumia wachache walio sahihi, watawavuta wengine wengi sahihi kuja kwako pia.

Kutokujikubali na kujiamini ndiyo chanzo cha watu kuhangaika ili wapendwe na kila mtu.
Kwa sababu mtu hajiamini mwenyewe, anachukulia kuchukiwa na wengine kama kuthalilisha nafsi yake.

Wewe usiwe hivyo, usiwe mtu wa kutaka uthibitisho kutoka kwa wengine, jijengee uthibitisho wako mwenyewe, kwa kujikubali na kujiamini.

Hakuna yeyote aliyefanikiwa sana ambaye alipoteza muda wake kuhangaika na kila mtu ampende.
Kila anayefanikiwa kimaisha anafanikiwa pia kutengeneza kundi kubwa la wanaomchukia.

Lakini kundi hilo halimsumbui hata kidogo, hapotezi muda na nguvu zake kuhangaika na watu wenye chuki. Kwa sababu anajua hakuna chochote anachoweza kunufaika nacho kutoka kwao.

Anza kuishi hivi hata kaka bado hujafika kwenye mafanikio makubwa. Usibabaishwe na yeyote asiyekupenda au kukukubali.
Maana wengi ambao wako tayari kukuchukia, wanajichukia wao wenyewe zaidi.
Sasa hebu jiulize una kipi cha kunufaika nacho kutoka kwa mtu anayejichukia mwenyewe?

Hakuna. Usipoteze nguvu na muda wako kwa watu hao.

Kocha.