Mawazo 10 ya kuingiza fedha kwa usomaji wa vitabu.

Kitu kimoja ninachoamini sana ni kwenye zama tunazoishi sasa unaweza kulipwa kwa chochote unachofanya.

Miezi michache iliyopita nilinunua simu mpya, wakati naiweka kwenye chaji ukaja ujumbe, ingiza kipato kwa kuchaji simu yako.

Mwanzo nilishangaa, lakini baadaye nikajiambia kipi cha kushangaa kutoka kwenye teknolojia.
Sikufuatilia tena kuhusu hilo, lakini nina uhakika kuna namna linafanya kazi.

Unaweza kujiambia kuna vitu huwezi kulipwa kwa kufanya. Lakini nikuambie tu, hakuna.
Watu wanalipwa kwa kila kitu.

Hapa nakushirikisha mawazo 10 ya kuingiza fedha kupitia usomaji wa vitabu.
Unaweza kujiambia nani akulipe kwa kusoma vitabu.
Lakini ukifungua macho na kuangalia, utaziona fursa nyingi.

  1. Kutumia yale unayojifunza ili kuongeza kipato zaidi.

  2. Kuandaa chambuzi za vitabu unavyosoma na kuwauzia wengine.

  3. Kuwa na blogu unayoshirikisha vitabu ulivyosoma na kuitumia kuingiza kipato.

  4. Kutengeneza video za chambuzi za vitabu unavyosoma na kuweka YouTube kisha kuingiza fedha kwa matangazo.

  5. Kuwa wakala wa vitabu unavyosoma na kuwashawishi wengine kuvinunua na kulipwa kamisheni.

  6. Kuanzisha klabu ya usomaji wa vitabu na watu kulipa ada kujiunga na klabu hiyo.

  7. Kuwa na duka la vitabu ambavyo unauza na kuweza kuwashawishi wateja kununua kupitia usomaji wako.

  8. Kuandaa tamasha au kongamano la kuhamasisha usomaji wa vitabu na kulipwa kwa njia mbalimbali kama matangazo, udhamini, uwakala n.k.

  9. Kuwashauri watu vitabu vya kusoma kulingana na mahitaji yao au ubobezi wanaotaka kujijengea na wakakulipa. Hapa pia unaweza kuwasimamia katika kujijengea tabia ya usomaji.

  10. Kushiriki mashindano mbalimbali ya usomaji na uchambuzi wa vitabu na kushinda fedha na zawadi nyingine.

Kama wewe ni msomaji mzuri wa vitabu, usiache kutumia fursa mbalimbali zilizopo za kuingiza kipato kupitia usomaji wako.

Kocha.